Na John Walter-Manyara
Kamati ya kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya UKIMWI imetembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara kukagua huduma za afya kwenye kituo cha tiba na matunzo kwa watu wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi CTC.
Akiongoza kamati hiyo kaimu mwenyekiti ambaye ni Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga baada ya kufanya ukaguzi hospitalini hapo, amesema ameridhishwa namna huduma zinavyotolewa na kuupongeza uongozi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara kwa kufanya kazi kwa weledi kwa kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa.
“Nawapongeza sana kwa sababu mmetunza ile amana yenu ya dawa, fedha zinazotolewa na serikali kwakweli hata sisi tumeridhika kwamba matumizi yake ni mazuri na muongeze juhudi hizo za kulinda huo mtaji na maeneo mengi tumekuta huduma kwa wagonjwa sio nzuri lakini hapa kwenu tumekuta wagonjwa wananyuso za furaha.” alisema Mtenga
Aidha mwenyekiti Hassan ametoa maoni ya kuboreshwa zaidi kwa huduma za matunzo kwa watu wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi CTC kuwa na usiri mkubwa ili kutoa fursa kwa wagonjwa kuwa huru kupata huduma na kuwarudisha walioacha kutumia dawa kwasababu hiyo ya kutokuwepo kwa usiri.
Naye Naibu Waziri wa afya Dkt Godwin Mollel ameishukuru kamati hiyo kwa kuona kazi kubwa inayofanywa na wizara ya afya ya kuboresha sekta ya afya nchini na kuahidi kufanyia kazi mapungufu machache yaliyojitokeza ikiwemo usiri wakati wa kutoa huduma kwa watu wenye maambukizi ya VVU ili huduma ziendelee kuwa bora zaidi na watanzania wanufaike na fedha zinatolewa na Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
“Tunaichukua kama changamoto na sio mara ya kwanza hilo kusemwa na mimi naamini litatusaidia sana kwenye watu kupotea kwani licha ya kwamba tumetenga sehemu za kuwahudumia kwahiyo wengine wanaona aibu kwenda” alisema Mollel
Awali akiwasilisha taarifa ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Katherine Magali amesema hospitali inatoa huduma za kibingwa zinazofanyika mara mbili kwa mwaka na kufanya usimamizi shirikishi wa kitaalamu ambapo kwa mwaka 2023 wamehudumia wagonjwa 47,000 kama wagonjwa wa nje na wagonjwa wa ndani 19,000 walilazwa.
DKT Katherine amesema kwa sasa wanayo idara 10 ambazo zinatoa huduma hospitali ya mkoa huku kukiwa na vitengo 20 kikiwemo kitengo cha tiba na matunzo CTC.
Imetimia miaka 11 tangu hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara ianze kutoa huduma mwaka 2013 na miaka 10 tangu ianze kufanya huduma za uapasuaji na kulaza wagonjwa mwaka 2014 na kwasasa inajumla ya watumishi 270 wa kuajiriwa na watumishi 65 wanaojitolea.
0 Comments