Sheria ya uhujumu uchumi kutua katika uvuvi

Dar es Salaam. Baada ya baadhi ya wavuvi kuendelea kuvua samaki kinyume na sheria ikiwamo samaki wadogo na wengine kutumia sumu, sasa Serikali imeamua kubadilisha sheria ili kutoa adhabu zaidi.



Wavuvi

 Kwa sasa ipo mbioni kufanya mabadiliko ya sheria zinazosimamia uvuvi kwa kuyaanisha baadhi ya makosa ya uvuvi haramu kuwa ni ya uhujumu uchumi, ili kuongeza adhabu kali kwa watu wanaotiwa hatiani.

 Hatua hiyo ya Serikali imekuja baada ya sheria na kanuni zilizopo kushindwa kupambana kikamilifu na vitendo vya uvuvi haramu vinavyotishia ukuaji wa sekta ya uvuvi nchini.

 Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amesema kuwa wataalamu wa wizara hiyo wamebainisha upungufu uliopo na kilichobaki ni kuwasilisha mabadiliko hayo mbele ya Bunge.

 Sekta ya uvuvi inasimamiwa zaidi na Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003 na Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 2009.

 Amesema vitendo vya uvuvi haramu havikomi licha ya Serikali kupambana navyo kwa kuwa adhabu zinazotolewa na sheria zilizopo haziwaogopeshi wavuvi haramu ambao shughuli zao huwaingizia mamilioni ya fedha.

 Dk Tizeba ambaye ni mhandisi kitaaluma, ametolea mfano wa tani 1.5 za samaki walizozikamata feri ya Dar es Salaam zikiwa zimevuliwa kwa mabomu na wavuvi hao kutoroka kuwa ni dalili za kutoogopa mkono wa sheria.

 “Baadhi ya samaki hao walivuliwa katika kina kirefu wakionyesha wavuvi hao wana uwezo mkubwa wa kifedha.

Lakini hawa ukiwapeleka mahakamani adhabu yao ni kifungo miezi sita au faini yao ni Sh200,000. Kiwango hiki ni kama unawaambia waende walipe ushuru wa Serikali kupitia Mahakama kwa sababu mzigo wanaovua ni mkubwa unaozidi hata thamani ya Sh18 milioni,” amesema.

 Mtaalamu wa masuala ya bahari kutoka shirika la kimataifa la WWF, Dk Mathias Igulu amesema uvuvi haramu unatishia mustakabali wa vizazi vijavyo kwa kuwa matumizi ya mabomu na sumu huaribu mazalia na makazi ya samaki.
Mpya zaidi Nzee zaidi