Mabomu yarindima wakizuia mahindi yaliyokamatwa na TRA

Kyela. Polisi wilayani hapa jana walitumia mabomu ya machozi kuwatanya wakazi wa Kijiji cha Kasumulu waliokuwa wakiwazuia askari na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukamata tani 30 za mahindi yaliyodaiwa kutoka Malawi na kuingizwa nchini kinyemela.

Mahindi hayo yalihifadhiwa kwa mkazi mmoja kijijini hapo na polisi walianza kuyaondoa eneo hilo ili wakayahifadhi kituoni, ndipo wananchi walipokusanyika kuwazuia.

Mfanyabiashara mwenye shehena hiyo, Japhet James alisema mahindi hayo ni mali yake na aliyanunua kwa watu mbalimbali kwenye vijiji vinavyozunguka Kasumulu.

“Mimi ni mfanyabiashara, nanunua mahindi kwa wananchi vijijini na wengine wananiletea ofisini kwangu, hivyo kusema yameingia kinyemela kutoka Malawi kama wanavyodai TRA, siyo kweli labda wanaoniletea na kuniuzia ndiyo wanatoa Malawi.”

Jana, kulizagaa taarifa kijijini hapo kwamba kuna malori yanayosafirisha mahindi ya msaada kutoka Umoja wa Mataifa kwenda Malawi na moja lilidaiwa kuchepuka.

 Ofisa Mfawidhi wa TRA, Kituo cha Kasumulu, Alex Misanga alisema walipata taarifa za kuingia mahindi kutoka Malawi kwa njia ya panya bila kulipiwa kodi, hivyo kuweka mtego.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula aliwaonya wananchi kuacha majaribio ya kuwazuia polisi au maofisa wa Serikali kutimiza wajibu wao wa kisheria.
Mpya zaidi Nzee zaidi