Wachezaji wa Simba
Simba ilimchezesha beki wake, Novalt Lufunga kwa kumjumuisha kwenye kikosi kilichocheza mchezo wa raundi ya tano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Polisi Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru, Simba ilishinda mabao 2-0.
Msimu uliopita katika mchezo wa robo fainali kati ya Simba na Coastal Union wa Kombe la FA, Lufunga alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa michuano hiyo, mchezaji huyo alitakiwa kukosa mechi mbili zilizofuata.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 22 (1) ya mashindano ya Kombe la Shirikisho inayozungumzia udhibiti wa wachezaji, inasema mchezaji atakayefanya jambo lolote kinyume na kanuni za nidhamu ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.
Kanuni ya 37(1) ya Ligi Kuu inasema, mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kadi mbili za njano hataruhusiwa kucheza mchezo mmoja unaofuata wa timu yake. Kifungu cha pili kinasema; Mchezaji atakayeonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja atakosa michezo miwili inayofuata.
Vifungu hivyo vya kikanuni vinaiweka Simba katika hatari ya kuondolewa kwenye mashindano hayo.
Meneja wa Simba, Mussa Hassan Mgosi akizungumzia kwa nini Simba ilimjumuisha Lufunga katika mchezo huo ilhali alikuwa na kadi nyekundu, alimtaka mwandishi kumuuliza kuhusu maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Azam.
“Tunajiandaa na Azam, mechi na Polisi tulishamaliza na tumesonga mbele. Tuzungumzie mechi dhidi ya Azam. Halafu mbona mnaandika sana kuhusu jambo hili, hakuna mengine?” alihoji Mgosi.
Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Jonas Kiwia alipoulizwa juu ya sakata hilo alisema: “kanuni zetu haziniruhusu kuzungumza chochote, wasiliana na Alfred
Lucas (Ofisa wa TFF), yeye anaelewa kila kitu na tayari tumeshampa mwongozo wa kulizungumzia suala hilo.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alipoulizwa alisema yuko mapuzikoni na kutaka msemaji wao (Alfred) ndiye aulizwe.
Alfred alipotafutwa alisema Kamati ya Rufani itakapokaa ndiyo itatoa majibu sahihi ya suala hilo.
“Ni vigumu kulizungumzia kwa sasa, tusubiri kamati ya rufani itakapokutana ndiyo itatoa mwafaka wa hili jambo,” alisema Lucas kwa kifupi.
Aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji, Mwanasheria Alex Mgongolwa alipoulizwa alisema sheria ni msumeno na adhabu zimewekwa ili atakayekiuka awajibishwe kulingana na vifungu. “Hizi kanuni zimetungwa na klabu zenyewe, hivyo kama ukiukwaji umefanyika ni kurudi kwenye kanuni zinasemaje na adhabu kuchukuliwa kulingana na kanuni,” alisema Mgongolwa na kuongeza.
“Kila kitu kiko wazi kama sheria inasema klabu ikimchezesha mchezaji mwenye kadi nyekundu ananyang’anywa pointi, kanuni ziko wazi sababu zimetungwa na klabu zenyewe, sheria itumike sawa sawa kwa kila timu.”
Viongozi wa Simba walipotafutwa kutoa ufafanuzi juu ya suala hili, Makamu Mwenyekiti, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ hakuwa tayari kuzungumza wakati simu ya rais wa klabu hiyo, Evance Aveva ikiita bila kupokewa.
Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alipoulizwa, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa kwani yuko kwenye mkutano na msaidizi wake, Kassim Dewji alisema yuko hospitali hawezi kulizungumzia pia.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa timu ya Polisi Dar, Inspekta Jordan Sampa alisema timu yake imewasilisha rufani dhidi ya mchezaji huyo kwenye kamati ya mashindano ya shirikisho hilo.
“Taratibu zinatutaka kukata rufaa si chini ya saa 72, tumesilisha rufani ili haki ipatikane, wao (kamati) watakaa kama wanaona rufaa yetu ina uhalali watakaa na kuyafanyia kazi,” alisema Inspekta Sampa.
Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alitaja mabadiliko ya makocha na kutotunza kumbukumbu kama tatizo linalozikabili klabu za soka nchini.
“Suala la utunzaji wa kumbukumbu ni la benchi la ufundi. Inawezekana kabisa kuna kukosekana kwa umakini wa kutunza taarifa za wachezaji na hili ni tatizo kwa klabu zetu. Pia, mabadiliko ya benchi la ufundi yanachangia,” alisema Mayay.
Kocha wa zamani wa Bandari ya Mtwara, Kenny Mwaisabula alisema ikiwa itabainika Lufunga alishiriki mchezo huo kimakosa TFF itabeba lawama kwa kuwa lina jukumu la kuzikumbusha klabu.
“Klabu zetu zina matatizo, lakini TFF walikuwa wapi kuwakumbusha (Simba), mbona CAF wana mfumo wa kuzikumbusha klabu kuhusu wachezaji wanaotakiwa kutumika kwa mchezo husika.”
