Simba yapotea njia kwenye mashamba ya miwa

Vinara wa ligi kuu Tanzania Bara imeanza kupoteza mwelekeo wa njia ya ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara baada ya leo kupotea njia kwenye mashamba ya miwa, na kulazimishwa suluhu na wakata miwa wa Mtibwa Sugar

Katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Jamhuri mjini Morogoro, Simba imeendelea kuonesha 'ubutu' katika safu yake ya ufungaji kwa kutengeneza nafasi nyingi lakini ikishindwa kuzitumia.

Kwa upande wa Mtibwa, waliingia uwanjani wakionesha kukamia mchezo huku wakiwa na mbinu ya kumaliza kwa sare kwa kuweka ukuta imara ulioongozwa na wakongwe Henry Joseph Shindika, Vincent Barnabas, Issa Rashid 'Baba Ubaya' na kiungo Shaaban Nditi, hali iliyopelekea mchezo huo umalizike bila bao kwa upande wowote.

Akizungumzia mchezo huo, Naohodha wa Simba Jonas Mkude amekubali matokeo na kusema mpira una matokeo matatu, hivyo licha ya kutoyapenda, inabidi wayakubali kwa kuwa ndiyo matokeo ya mpira, na kuahidi kufanya vizuri zaidi katika michezo inayofuata.

Kwa upande wake Nahodha wa Mtibwa Sugar Shaaban Nditi ameshukuru kupata point moja katika mchezo huo, huku akitupia lawama ubovu wa uwanja na kusema wao hawakuzoea kufanya mazoezi katika uwanja huo, hivyo ubovu wa uwanja umechangia kuikosesha timu yake ushindi katika mchezo wa leo.

Matokeo haya yanaifanya Simba iendelee kubaki kileleni kwa kufikisha point 45, ikiwa ni point 2 mbele ya Yanga

Simba na Mtibwa ni timu ambazo wachezaji wake wengi wamewahi kuzichezea timu zote mbili yaani kuna wachezaji wa Simba waliotoka Mtibwa na kuna wachezaji wa Mtibwa waliotoka Simba, hivyo ni timu ambazo wachezaji wake wengi wanafahamiana

JIUNGE NASI 
 INSTA@MUUNGWANABLOG ,FB@MUUNGWANABLOG,YOUTUBE @MUUNGWANA TUBE, BOFYA HAPA KU-INSTALL APP YA MUUNGWANA BLOG ILI UPATE URAHISI KUZISOMA HABARI ZOTE KWA WAKATI.
Mpya zaidi Nzee zaidi