
Serikali imepiga marufuku uvutaji wa shisha nchini, ikiwa ni mkakati wa kuzuia matumizi ya dawa za kulevya. Kwa kawaida shisha huvutwa kwa kutumia mirija iliyounganishwa kwenye mitungi ambayo huchuja moshi unaotoka sehemu ambayo tumbaku inachomwa.
Ni kama vile uvutaji kiko isipokuwa moshi wa shisha hupitishwa kwenye mitungi maalumu. Pamoja na kwamba shisha inaruhusiwa maeneo mengi duniani na hasa kwenye hoteli kubwa, jijini Dar es Salaam uvutaji ulikuwa ukifanywa vibaya kutokana na wauzaji kuchanganya na dawa za kulevya.
Vitendo hivyo vilifanya Serikali ipige marufuku uvutaji shisha. Lakini ni kweli shisha haivutwi baada ya amri hiyo? Mwandishi wetu, Jackline Masinde anafuatilia swali hilo kwa kutembelea maeneo aliyohisi kuna biashara hiyo. Fuatana naye katika habari hii iliyoandikwa kwa mtindo wa simulizi...
Kuna mistari ya kibwagizo cha wimbo uliowahi kuimbwa na msanii wa nyimbo za kizazi kipya maarufu kama Bongo fleva, Babu Kitale unaoitwa ‘Dude’
Mistari hiyo inasema,... “Hili dude noma masela hili dude nomaaa... hili dude noma masela mbona mtakoma...”
Mistari hii inatoa ujumbe kwa hadhira juu ya athari ya kutumia dawa za kulevya, ambazo msanii huyo ameziita kwa jina la “dude” akitumia neno “masela” kumaanisha “ndugu zangu” au “jamani”.
Kwa maana nyingine, msanii huyo angeweza kuimba wimbo huo kwa lugha nyepesi kwa kusema “hii shisha ni mbaya sana, hii shisha ni mbaya jamani, mbona mtakufa?”
Ni kweli, kilevi aina ya shisha, kinachovutwa kwa kutumia mirija iliyounganishwa kwenye mitungi ambayo huwekwa tumbaku na kuchomwa moto, ni hatari.
Ni kama uvutaji wa kiko kwa kuwa hutumia tumbaku ya kawaida ambayo moshi wake hupitishwa kwenye mitungi na baadaye mrija mrefu ambao mvutaji huutumia kuvuta moshi.
Kwa kawaida shisha haileweshi, bali huchangamsha mwili, lakini nchini inatumiwa vibaya; huchanganywa na dawa za kulevya ili kuongeza msisimko zaidi.
Kutokana na mbinu hizo za kuongeza msisimko kwa kutumia dawa zilizopigwa marufu, uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam umepiga marufuku matumizi ya shisha, na hasa uvutaji kwenye klabu kubwa, hotelini na mitaani.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameshapiga marufuku na hata kuwatuhumu viongozi wa vyombo vya dola walio chini yake kuwa huenda kuna kitu wanafanya ndiyo maana wanasita kushughulikia tatizo hilo.
Lakini marufuku hiyo inaonekana kupuuzwa kwenye baadhi ya maeneo, ingawa kwa kiasi kikubwa imedhibitiwa.
Shisha iko wapi Dar
Nikiwa nataka kujua ukweli wa matumizi ya shisha, nikaingia kazini kuisaka ilipo ili kujiridhisha kama wahusika wametii agizo la Serikali ya mkoa wao.
Katika uchunguzi wangu nilibaini baadhi ya maeneo kuwa bado yanaendelea na utumiaji wa shisha kama Ubungo Darajani, ambako kuna genge la mateja ambao huchanganya shisha na bangi.
Eneo jingine ni Coco Beach, ufukwe unaotumiwa bure na wakazi wa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupunga upepo, kuogelea na burudani nyingine za muziki.
Eneo jingine ni Mnazi Mmoja ambako kuna sehemu imebatizwa jina la Kwa Mhindi kunakouzwa kilevi hicho na hali kadhalika kwenye hoteli moja maarufu ya muda mrefu jijini Dar es Salaam, ambayo jina tumelihifadhi kwa sababu za kiufundi.
Aidha, nilimtafuta mmoja wa wafanyabishara ya shisha kutoka Terrace Lounge na mtumiaji mmoja wa shisha.
Shisha inavutwa Dar
Saa 12:00 jioni nilianza safari ya kwenda Coco Beach na baada ya saa moja tuliwasili na kukuta watu wengi.
Dereva teksi niliyokodi ambaye ni mwenyeji wa Coco Beach, ananipeleka hadi eneo ambalo shisha inauzwa.
Sehemu hiyo ina meza ambayo hutumiwa na wavutaji ambao wakati huo hawakuwepo. Hakukuwa na dalili zozote za watu kuwepo zaidi ya hiyo meza.
Pembeni yake, walikuwapo watu waliokuwa wakiburudika kwa vinywaji na vyakula.
“Hapa ndipo huwa wanauza (shisha). Kila ninapokuja Coco Beach nakuta vijana wengi wamekaa kwa makundi eneo hili wakivuta,” anasema dereva huyo.
“Kwani sasa hizi ni saa ngapi?” ananiuliza.
“Ni saa 4:55 (usiku),” namjibu baada ya kuangalia saa yangu ya mkononi.
“Basi ndo maana tusubiri mpaka ifike saa 6:00 usiku. Muda huo ukifika, watu huja hapa kuvuta. Saa hizi tumewahi sana,” anasema dereva.
Baadaye tukaanza kuzunguka eneo la Coco Beach na kunagalia kama kuna sehemu nyingine wanauza. Kulikuwa na vijana waliokuwa kwenye makundi na wengine hadi kwenye kingo za bahari, wakionekana kutokuwa na hofu licha ya usiku kuwa mwingi.
“Hawa vijana si watakuwa wanafunzi na wana wazazi. Iweje wako huku mpaka sasa?” Ndivyo nafsi yangu ilivyouliza.
Sikuweza kupata jibu mpaka nilipoamua kumuuliza dereva swali hilo.
“Wengi wao hapo ni wanafunzi wa chuo,” alijibu dereva wangu.
Tayari ilishafika saa 6:00 usiku na hivyo tukaamua kujongea eneo ambalo Shisha inauzwa.
Pia hatukukuta chochote. Niliangaza macho huku na kule, lakini sikupata. Nikaamua kumuita mhudumu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Neema.
“Mambo dada? Naomba kuuliza shisha inapatikana hapa?”
“Ndiyo shisha ipo pandisha kule juu. Hapa siku hizi hawauzi wanaogopa kukamatwa,” alijibu Neema. Nilielekea sehemu ambayo Neema alinielekeza. Sehemu hiyo kuna baa, juu na chini eneo hilo la Coco Beach.
Juu ndiko walikokuwa wakivuta shisha na chini kulikuwa na burudani ya muziki na ili kuingia ndani lazima ulipe mlangoni.
“Dada vipi, leta pesa,” anasema kijana aliye mlangoni ambaye amejengeka misuli, nadhani kutokana na mazoezi ya kubeba vitu vizito.
Aliniambia kama nataka kuingia nilipe Sh5,000.
Nilitoa fedha hizo na kuingia ndani ya ukumbi ambako ninakuta watu wakifurahi na kucheza muziki unaotumbuizwa na bendi.
Nikiwa chini ya ukumbi huo, kwa juu ninaona watu wakiwa wamekaa huku moshi ukifuka kutoka eneo lao.
Mwanzoni nilihisi ni moshi wa sigara, lakini nilipoangaza vizuri nikaona si moshi wa kawaida wa sigara ambao nimezoea kuuona.
Lakini nikaamua kuendelea kukaa kidogo kuangalia burudani kutoka bendi hiyo huku nikipiga akili ya kwenda eneo hilo lenye moshi kushuhudia vizuri.
Huku nikiwa na hofu ambayo sijui ilitoka wapi, nikajivuta taratibu kuelekea juu. Wakati najaribu kupanda ngazi ya kwanza, nikasikia sauti ikiuliza:
“Wewe unaenda wapi huko?”
Niligeuka kuona nani ananiuliza. Alikuwa kijana aliyekuwa amevalia fulana isiyo na mikono, maarufu kama vesti na iliyo na mistari ya rangi nyeupe na nyekundu.
Huyu ni kijana mfupi wa wastani na mweusi.
Itaendelea kesho