ZACHARIA HANSPOPE.
SIKU chache baada ya Simba kuondolewa kwenye usukani wa ligi, klabu hiyo imesema haina hofu na kurejea tena kileleni kwa kuwa bado kuna idadi kubwa ya mechi zilizobaki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope, alisema kuwa ni 'kichekesho' kukata tamaa wakati bado wana michezo 10 mbele yao.
Alisema Simba bado ipo kwenye mbio za ubingwa na bado ina nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu licha ya kuwa imeshushwa kileleni na Yanga.
"Tuna utofauti wa pointi moja tu, na bado kuna michezo 10 imebaki kwa nini tukate tamaa, hao waliokaa kileleni sasa hivi nao wanaweza pia wakapoteza mchezo, ndio mpira ulivyo," alisema Hanspope.
Alisema mashabiki wanaokata tamaa sasa hivi na kuongea mabaya juu ya Simba hawana ufahamu na mchezo wa soka.
Alisema hakuna sababu ya nje ya Uwanja iliyopelekea Simba ikafungwa mchezo wake dhidi ya Azam wiki iliyopita.
"Tulifungwa katika hali ya mchezo tu, tulipata nafasi hatukuzitumia wenzetu walitumia makosa ya beki wetu wakapata goli, hakuna sababu nyingine ya nje ya uwanja, watu waache kuongea vitu ambavyo havipo," aliongezea kusema Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Usajili.
Alisema kwa sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Majimaji utakaochezwa Jumamosi hii mjini Songea.
VIDEO: MKONDA AKIWATAJA TID, WEMA, HAMIDU, PETITI MAN, RECHO WANAHUSIKA NA MADAWA YA KULEVYA.
