Kiwanda kimepigwa faini mil. 25/- kwa kutiririsha maji machafu

KIWANDA cha Chemicotex kilichopo eneo la Africana Mbezi Beach, Dar es Salaam kimepigwa faini ya Sh. milioni 25 kwa kosa la utiririshaji wa maji machafu yenye kemikali kwenye mfereji wa kupitisha maji ya mvua.

Chemicotex kinazalisha bidhaa mbalimbali zikiwamo mafuta ya kupikia, dawa ya mswaki, vipodozi na juisi.

Kadhalika, serikali imewataka wawekezaji kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni za mazingira katika kusimamia shughuli zao na kwamba hawatamfumbia macho atakayekiuka sheria.

Hatua hiyo ilichukuliwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina, akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa viwanda na kusema faini hiyo inatakiwa kulipwa ndani ya siku 14 kuanzia jana.

Mpina alisema lengo la kukitembelea kiwanda hicho ni kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kutiririshiwa majitaka katika makazi yao na kwenye biashara.

Aidha, Mpina alisema kwa kipindi kirefu amekuwa akifanya ziara kwa ajili ya ukaguzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye viwanda kwa lengo la kuwahatarisha wawekezaji kulinda mazingira.

Mpina alisema katika uwekezaji uwe wa ndani ya nchi ni lazima wawekezaji walinde mazingira na afya za wananchi wanapofanya uwekezaji wao.

Alisema sheria ya mwaka 2004 inazuia kiwanda, mgodi ama mtu yeyote kuharibu mazingira, kuhatarisha afya za watu na viumbe hai.

“Tutaendelea kusimamia maagizo yetu, kuna wengine wameshazoea viongozi kule nyuma walikuwa wanatoa maelekezo, lakini hawayasimamii, sasa wanatakiwa kujua hii ni serikali nyingine, tunasimamia yale tuliyoyaagiza hatutakiwi kuwa na wawekezaji ambao ni mzigo kwa Taifa na kusababisha athari kubwa kwa wananchi wetu,” alisema na
kuongezea:

“Tunapowaelekeza wawekezaji tunaomba watuelewe kwa nia njema, tupo kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi na uwekezaji ni lazima uwe rafiki kwa maisha ya wananchi,” alisema.

Aidha, Mpina alisema kiwanda hicho kinatakiwa kuhakikisha kinasafisha mfereji huo na kusitisha mara moja kutiririsha majitaka yanayosababisha uchafuzi wa mazingira.

Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Heche Manchare, alisema kiwanda hicho kinatiririsha maji machafu kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Manchare alisema kiwanda kinatengeneza zaidi ya bidhaa 20 ambazo zimekuwa na kemikali mbalimbali, hivyo maji yanayotoka ndani ya kiwanda hicho yanaweza kuwa na madhara kwa binadamu kwani yanaingia moja kwa moja baharini bila kuyatibu.

Alisema wamekuwa wakifika katika kiwanda hicho na kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakieleza jinsi kinavyofanya uchafuzi wa kupitisha maji taka kwenye sehemu ya kutolea maji ya mvua.
Mpya zaidi Nzee zaidi