Mahakama sasa kuanza kutembea

Dar es Salaam. Mahakama nchini iko kwenye mikakati ya kuanzisha korti maalumu zinazotembea kwa ajili ya kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususani waliopo kwenye maeneo ambayo hayana huduma hiyo.

Mkakati huo ulibainishwa jana na Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma wakati akifunga maonyesho ya wiki ya utoaji elimu ya kisheria katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Jaji Juma alisema kuna kata 3,957 ambazo zinapaswa kuwa na mahakama za mwanzo, lakini kwa sasa zipo 976.

Alisema kutokana na hali hiyo kuna haja ya kubuni utaratibu mwingine ili kuhakikisha wananchi kama vile wafugaji na wavuvi walioko visiwani wanafikiwa na mahakama ambayo itawasaidia.

“Kwa hiyo suala lingine ambalo kwa mwaka huu mahakama itahakikisha inalifanya ni kuanzisha mahakama ndogo zaidi (small claims court) ambazo zitajaribu kuwafikia watu ambao kwa sasa hawafikiwi na mahakama za kawaida,” alisema Jaji Juma na kuongeza:

“Katika nchi za Kenya na Uganda tayari zina mahakama zinazotembea ambazo ni muhimu, mwaka ujao tujaribu kuwa nazo.”

Akizungumzia mpango wa kuanzisha mahakama ndogo, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), John Seka alisema wamelipokea suala hilo kwa kuwa limekuwa kwenye mchakato muda mrefu.

“Kumekuwa na huo mchakato wa kuhakikisha kwamba haya mashauri madogo madogo ambayo hayaendi kwenye mambo ya kiufundi wa kisheria hayaingii kwenye mahakama za kawaida,” alisema Seka.

Aliongeza kuwa kuna masuala yanayohusu matunzo ya watoto, mirathi ndogondogo, wosia, kugombania ardhi ambayo hayahitaji ufundi mkubwa yanaweza kushughulikiwa ipasavyo kupitia mfumo huo.

“Sasa yakiingia kwenye mahakama za kawaida yanachukua muda mrefu,” alisema.

Alifafanua kuwa katika mahakama ndogo kwa kuwa zina kanuni na taratibu ambazo ni rahisi zaidi kushughulikia kesi hizo, zitasaidia kuondoa mlolongo wa mashauri mahakamani.

Mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam aliyejitokeza katika maonyesho hayo, Richard Msilanga alisema ni muhimu kwani hutoa elimu ya mambo mengi na muhimu.

Msilanga alisema kuwa amekuwa akihudhuria katika maonyesho hayo na kwamba, mara nyingi huwa anajifunza mambo mengi kwani hupata fursa ya kuuliza maswali kuhusu mambo mbalimbali ya kisheria.

Hata hivyo, alisema utaratibu wa taarifa kuhusu maonyesho hayo unapaswa kuboreshwa kwa kutolewa matangazo mapema kabla ya siku ya uzinduzi.





VIDEO: MJANE AMWAGA MACHOZI MBELE YA RAIS MAGUFULI KATIKA SIKU YA SHERIA.



Mpya zaidi Nzee zaidi