Mbaroni kwa kukutwa na jino la tembo

Kigoma. Polisi mkoani Kigoma wanamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kukutwa na jino la tembo lenye uzito wa kilo 15 akiwa katika harakati za kwenda kuuza nchini Burundi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Februali 6, kwenye basi la Saratoga lililokuwa likisafisha abiria kutoka Tabora kuelekea Kigoma.

Mtui alisema mtuhumiwa huyo aligundulika baada ya abiria mmoja wa basi hilo kudai kaibiwa simu, ndipo kondakta alitoa taarifa kituo cha polisi cha ukaguzi wa mizigo kilichopo Kijiji cha Kazulamimba Wilaya ya Uvinza.

Alisema polisi waliofanya upekuzi kwenye basihilo walikuta jino hilo likiwa limekatwa vipande vitatu. “Wakaguzi walipopekua begi la nguo la mtuhumiwa walibaini ndani kuwamo mfuko mweupe wa sandarusi uliozungushiwa kamba za mpira na walipofungua wakakuta vipande vitatu vya nyara hiyo ya Serikali,” alisema Mtui.

Ofisa wanyamapori wa Mkoa wa Kigoma, Idd Salum alisema tembo huyo aliyeuliwa inawezekana ni wa Hifadhi ya Katavi ya mkoani Katavi au wa za Seruu kwa kuwa hifadhi za Mkoa wa Kigoma hazina tembo wenye meno makubwa kama lililokamatwa.
Mpya zaidi Nzee zaidi