Tanesco kujenga mradi wa kufua umeme wa Megawati 87 kwa kutumia maji ya mto Kagera.

Mradi mkubwa wa kufua umeme wa megawati 87 kwa kutumia maji ya mto Kagera unatarajiwa kujengwa na shirika la ugavi wa umeme nchini ( TANESCO ) katika kijiji cha Kakono wilaya ya Misenyi mkoani Kagera kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 7.8.

Mratibu wa mradi wa Kakono kutoka makao makuu ya shirika la umeme nchini Stanslaus Kizzy, amewaeleza wajumbe wa bodi ya maji bonde la Ziwa Victoria waliotembelea mahali mradi huo unapotarajiwa kujengwa kuwa pindi ukikamilika utaongeza zaidi ya megawati 70 kwenye gridi ya taifa na hivyo kuifanya mikoa ya kanda ya ziwa kuwa na umeme wa uhakika zaidi.Kaimu Afisa wa maji bonde la Ziwa Victoria Mangasa Ogoma Nyamhanga amewashauri watumiaji wa maji kuhakikisha wanatekeleza sheria ya maji namba 11 ya mwaka 2009 ili kuepusha migogoro ikiwemo pia kulinda na kutunza vyanzo vya maji kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya maji bonde la Ziwa Victoria Prof. Philip Bwathondi amelishauri shirika la umeme nchini pamoja na wadau wengine kuwa na cheti cha tathimini ya athari ya mazingira kabla ya mchakato wa kumpata mhandisi mwelekezi na mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo.

Mradi wa kufua umeme wa Kakono uliopo jirani na kiwanda cha sukari Kagera uliibuliwa mwaka 1970 na upembuzi yakinifu wa mradi huo ulikamilika mwaka 2014, mikoa mitano ya kanda ya ziwa kwa sasa inatumia umeme wa jumla ya megawati 106 kutoka kwenye gridi ya taifa pamoja na ule wa kutoka Uganda kwa ajili ya mkoa wa Kagera, ambapo megawati 60 za Nyakato Mwanza za umeme unaotumia mafuta zinachangia pia kwenye gridi ya taifa. Matumizi  ya umeme kwa mkoa wa Kagera peke yake ni megawati 18.
Mpya zaidi Nzee zaidi