Watu wawili wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa kwa risasi baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kuteka basi.

Watu wawili wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa kwa risasi baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha kuteka basi dogo la abiria lililokuwa likitokea kijiji cha Kitanga kilicho mpakani na Burundi kwenda Kasulu mjini, tukio ambalo limepelekea kukamatwa kwa wahamiaji haramu 168 kijijini hapo.

Tukio hilo limetokea alfajiri wakati basi hilo likielekea mjini kasulu ambapo lilishambuliwa kwa risasi na kulazimika kusimama ambapo watekaji walipora mali kadhaa za abiria pamoja na pesa taslim zaidi ya shilingi laki tisa huku abiria Alex Daud na India nyanda wakipoteza maisha baada ya kupigwa risasi kama wanavyoeleza baadhi ya wananchi.

Baada ya tukio hilo kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kigoma ikiongozwa na mkuu wa mkoa wa kigoma Brigedia jenerali mstaafu Emmanuel Maganga imefika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata watu 168 ambao ni raia toka burundi wakiishi katika kijiji hicho kinyume cha sharia ambapo kamanda wa polisi Kigoma Ferdinand Mtui amesema kati ya watu hao tisa wametambulika kuhusika katika utekaji huku mkuu wa mkoa wa Kigoma akiwahakikishia wananchi kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo yote.
Mpya zaidi Nzee zaidi