SERIKALI wilayani hapa imewataka wafugaji kujenga nyumba za kudumu na kuwaagiza waache ufugaji wa kuhamahama, vinginevyo itawachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kutafukuza wilayani hapa.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happyness Seneda, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza wafugaji walioko wilayani mwake na kuwataka pia waache vitendo vya ubabe kwa wakulima.
Seneda alisema wilaya imetenga vijiji 24 kwa ajili ya wafugaji, hivyo hatarajii kuona au kusikia kwamba wanaendelea kuhamahama kwa vile tayari wameshapewa maeneo ya kuendeshea shughuli za ufugaji.
"Ninataka mjenge nyumba za kudumu na nitakuja kuwakagua. Kama nitakuta hakuna nyumba hizo nitawatimua, kwa sababu sitaki kuona mnaendelea na ufugaji wa kuhamahama kwa sababu hauna faida," alisema Seneda.
Aliwataka pia wafugaji hao kuunda vikundi vya ushirika kila kijiji kwa ajili ya kusimamia maeneo yao na kuyaendeleza ikiwa ni pamoja na kujenga majosho, uzio, kuchimba visima virefu na kupanda majani ya kulishia mifugo yao.
"Nirudie tena kwamba kujenga makazi ya kudumu ndiyo njia pekee ambayo itawafanya muache kuhamahama, hivyo baada ya kupangiwa maeneo ambayo mmepewa sitakubali kusikia au kuona mmehama," alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Magembe Makoye, aliipongeza serikali ya wilaya hiyo kwa kutenga maeneo ya wafugaji na kuwaomba viongozi wa wilaya zingine nchini kuiga mfano huo.
Alisema ana uhakika wafugaji wa wilaya hiyo hawatahama tena kwa vile wameshapata maeneo ya kufugia na kwamba wafugaji wakiitumia vizuri fursa hiyo watafaidika na mifugo yao.
"Kwa niaba ya wafugaji sina budi kuipongeza serikali ya wilaya ya Kisarawe kwa kutambua shida ya wafugaji na kuitafutia ufumbuzi, hivyo niombe wilaya zingine kuiga mfano huu," alisema Makoye.
Katibu huyo aliwataka wafugaji kuzingatia maelekezo na dhamira njema ya serikali kwa kujenga nyumba za kudumu katika maeneo waliopewa ili wasiendelee kuhamahama.
Kwau pande wake, mmoja wa wafugaji hao, Dotto Mabula alisema bado elimu kubwa inahitajika ili kuhakikisha kwamba wafugaji wanaachana na mtindo wa kuhamahama kwa vile wengi wao ni wagumu hubadilika kulingana na wakati.
Alisema iwapo watapewa elimu na kubadilika, changamoto zinazowakabili kwa sasa zitakwisha kabisa na watafaidika na mifugo yao badala ya sasa kwa kuwa ni wachungaji badala ya wafugaji.