Bocco kurejea uwanjani karibuni

JOHN BOCCO

NAHODHA wa mabingwa wa Kombe la Kagame Azam FC, John Bocco, ameanza mazoezi na huenda akarejea uwanjani kuitumikia timu hiyo kabla ya kumalizika kwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara imefahamika.

Hata hivyo Bocco hakusafiri na kikosi cha timu hiyo ambacho leo kitashuka dimbani kuivaa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa CCM , Mkwakwani jijini Tanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa Azam FC, Jaffer Iddi, alisema kuwa benchi la ufundi la timu hiyo liliamua kumuacha mshambuliaji huyo kwa sababu hajakuwa 'fiti' kucheza mechi za ushindani.

Idd alisema kuwa wamefurahi kuona kiungo Salum Aboubakar amepona na anaweza kupangwa katika kikosi kitakachocheza leo.

"Hatutaki kumrejesha haraka Bocco, tunataka apone na atakapoingia uwanjani acheze soka la ushindani, bado tuna mechi muhimu za Kombe la FA, pia hata ligi haijamalizika, lolote linaweza kutokea," alisema kiongozi huyo.

JKT Ruvu inaburuza mkia katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 22 wakati Azam FC wao watashuka uwanjani wakiwa kwenye nafasi ya tatu kutokana na kujikusanyia pointi 45.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items