Baada ya Kupasua Maiti na Kuchukua Kete za Madawa, Wafanyakazi wa Mochwari watiwa Mbaroni

WAFANYAKAZI wanne wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya upasuaji kwenye mwili wa maiti na kuchukua madawa ya kulevya kisha kuyauza madawa hayo.

Akizungumza na wanahabari mapema leo (Mei 26, 2017), Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Simon Sirro amesema;

“Yule Mghana aliyekutwa amefariki dunia Machi 14, 2017 katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Red Carpet iliyopo Sinza, alichukuliwa kupelekwa Mwananyamala Mochwari (chumba cha kuhifadhia maiti), lakini wale wafanyakazi wa kwenye ile mochwari nafikiri walipata taarifa kuwa mwili ule una madawa ya kulevya, hivyo walifanya njama wakapasua ule mwili na kutoa kete 32 za madawa ya kulevya ambayo kimsingi waliyauza.

“Baada ya jeshi la polisi kuwahoji wamekiri kwamba ni kweli walihusika kuupasua mwili huo na kuchukua kete za madawa, baada ya hapo waliyauza madawa na huyo waliyemuuzia tumekwishamkamata.

Sirro alienda mbele zaidi na kueleza;

“Huyo aliyeuziwa naye alikwenda kumuuzia jamaa mmoja anayeitwa Ally Nyundo ambaye yumo kwenye orodha ya wauza madawa waliotajwa na Mkuu wa Mkoa, na tulishawahi kumpeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali akabainika anatumia madawa ya kulevya.

“Kwa hiyo mpaka sasa tunawashikilia watuhumiwa watano wa tukio hilo ambapo wanne ni wahudumu wa hiyo mochwari na mmoja ni yule waliyemuuzia kete hizo za madawa, hivyo tunaandaa jarada kwa ajili ya kulipeleka kwa wakili wa serikali” alisema Sirro.

Tazama Video hii .