Yule shabiki wa Simba kuzikwa Moshi, Alhamisi

Hii ndiyo gari iliyochukua uhai wa Shose (picha ndogo juu kulia)

MWILI wa marehemu Shose Fidels Alhamisi utasafirishwa kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yaatakayofanyika Ijumaa.

Taarifa ya familia ya marehemu imesema kwamba mwili wa mpendwa wao, Shose utaagwa mapema Alhamisi kabla ya safari ya kuelekea Moshi tayari kwa maishi yake Ijumaa, ambayo yatafanyiak Uru.
Shose alifariki dunia Jumapili mchana, muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya mkoa wa Morogoro, kufuatia ajali ya gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 eneo la Dumila mkoani Morogoro.

Binti huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 na ushei, alikuwa pamoja na Nahodha wa Simba, Jonas Mkude kwenye gari hilo na watu wengine, wakitokea Dodoma, ambako jana timu yao ilitwaa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa ushindi 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Jamhuri.

Ndani ya gari hilo walikuwepo pia wapenzi wengine wa Simba, Jasmin na Faudhia ambao wameumia na wamelazwa hospitali ya mkoa wa Morogoro na hali zao zinaendelea kuimarika.

Mkude alirejeshwa Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi katika hospitali ya Muhimbili kabla ya mapema Jumatatu kuruhusiwa, wakati dereva ambaye pia ndiye mmiliki wa gari ajulikanaye kwa jina la utani, Rais wa Kibamba anaisaidia Polisi.