Kubenea amchongea Msaidizi wa Muhongo wa kwa Magufuli



SEAD Kubenea Mbunge wa Ubungo,  (Chadema), ameushauri uongozi wa juu wa serikali kumwajibisha Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, akidai kuwa amehusika na changamoto zilizomng’oa aliyekuwa waziri katika wizara hiyo, Prof. Sospeter Muhongo.

Kubenea aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana, alipokuwa anachangia mjadala wa makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao
wa fedha.

“Rais amemtumbua Waziri wa Nishati na Madini Prof. Muhongo. 'Why' (kwa nini) Muhongo amefanywa mbuzi wa kafara? Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ametumbuliwa, Naibu Waziri huyu hapa, naye awajibike. Kwa nini wameondolewa hao yeye amebaki?” alihoji.

Alibainisha Naibu Waziri huyo amefanya kazi kwenye wizara hiyo tangu mwaka 1999 alipomaliza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akiwa mwanasheria na amekuwapo huko mpaka alipopata Shahada ya Uzamivu.

“Sasa kama tunataka kumtoa Muhongo kafara, ni lazima Naibu Waziri awajibike. Ni lazima tujenge msingi katika taifa hili. Hatuwezi kuwa na 'double standard", alisema.

Kutokana na kauli hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, aliomba kumpa taarifa Kubenea akilieleza Bunge kuwa katika utendaji wa serikali, anayeshika dhamana kwenye wizara ni waziri na anawajibika kwa majukumu yote.

“Maana sisi (manaibu waziri) tunapojibu tunasema kwa niaba ya waziri mwenye dhamana, lakini pia mzungumzaji akumbuke historia ya baraza lililovunjwa na Rais (Ali Hassan) Mwinyi ni kwamba wawaziri peke yao ndio walitolewa na manaibu mawaziri walibaki,” alisema Dk. Kigwangala.

Akizungumzia taarifa hiyo ya Dk. Kigwangala, Kubenea alisema Naibu Waziri huyo hana uzoefu na hiyo ni awamu yake ya kwanza kuingia kwenye serikali, hivyo hawezi kupokea taarifa yake.

Hata hivyo, Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, alisimama na kuomba kumpa taarifa Mbunge huyo akieleza kuwa Dk. Kalemani asilaumiwe kwa kuwa hakuwa na sauti kwenye uamuzi wa masuala ya wizara.

“Alifika pale akitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuajiriwa kama Ofisa Sheria Daraja la II, hivyo alikuwa chini ya mtu, lakini baadaye aliondoka na kwenda kusoma PhD na mwaka 2014 akapandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Sheria, hivyo hakuwa na mamlaka kwenye hili,” alisema Kakunda.

Baada ya kuruhusiwa kuendelea kuchangia huku Spika Job Ndugai akiahidi kumlinda, Kubenea alisema anazungumzia Dk. Kalemani ambaye amekuwa mwanasheria katika Wizara ya Nishati na Madini na kwamba hiyo ndiyo hoja yake.

Alisema hana maslahi yoyote na Prof. Muhongo na hana mazoea naye hata kusalimiana, lakini katika hilo asiwe mbuzi wa kafara na kwamba serikali iende mbele zaidi kuangalia ilipojikwaa.

“Muhongo anasimamia mamlaka ya nishati na madini, waliokuwa viongozi kwenye wizara hiyo wakati huo na sasa na mikataba hii haikufungwa jana," alisema.

"Kwa mujibu wa rekodi zilizopo mwaka 1993, serikali ilipitisha muswada bungeni wa kuwaruhusu wawekezaji kusafirisha dhahabu, kupata misamaha ya kodi, kuondolewa VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) na kuondoa mchanga unaozalishwa kusafishia nje,” alisema Kubenea.

Alisema hakuna mtu anayepinga juhudi za Rais John Magufuli za kuokoa rasilimali za nchi ambazo zilikuwa zinafanywa kama shamba la bibi.
“Hoja yangu hapa ni kwa nini hatuzungumzii kitendo cha ndege kubwa kubeba dhahabu na tunajadili mchanga?” alihoji.

"Mchanga una dhahabu lakini maamuzi (uamuzi) yanayofanyika yanaweza kuliingiza taifa kwenye mgogoro mkubwa wa kidiplomasia, kisheria na kimahakama.

Pia, Spika wewe unakumbuka Bunge hili wakati wa sakata la Dowans tulishtakiwa mahakamani, tumelipa mabilioni ya shilingi na leo Tanesco ambayo iko makao makuu ya jimbo langu la Ubungo imeshtakiwa mahakamani na Benki ya Standard Chartered na inatakiwa ilipe mabilioni ya shilingi kwa fedha za Escrow ambazo waheshimiwa wabunge walikataa zisigawanywe humu ndani,” alisema.

Kubenea alisema kuna mawaziri na baadhi ya watendaji wakuu wa serikali wanakuwa na maslahi katika mikataba ya nchi na wamekuwa wakikaa kwenye baraza la mawaziri, kumbe nje wana kampuni zao za mifukoni au ya marafiki zao na kuiingiza nchi kwenye mgogoro.

“Bunge hili lilipitisha uamuzi kwenye Bunge la Tisa mwezi wa nane (Agosti) mwaka 2008 juu ya Richmond, maazimio ya Richmond hayakutekelezwa kama yalivyotakiwa. Kuna mtu anaitwa Bashir Mrindoko, alikuwa Kamishna wa Nishati pale Wizara ya Nishati na Madini, alitajwa miongoni mwa watu wanaopaswa kuwajibishwa na Rais mwaka 2008.

"Mwaka 2010 Bashir J. Mrindoko alitoa kibali kwa Kampuni ya Singida Wind Power Project Limited iendeshe umeme wa upepo wa Singida, huyu alikuwa Kamishna wa Nishati, miongoni mwa watu wanaomiliki hiyo kampuni na wengine wamo humu ndani (bungeni),” alisema akimtaja Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), kuwa mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo na alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco.

“Katika mazingira haya, taifa hili linawezaje kupata mikataba mizuri… Rafiki yake mkubwa ambaye wakati anaumwa alikuwa msemaji wa familia, Dk. Harrison Mwakyembe, alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba, mikataba yote inapitia kwake.

"Dk. Mwakyembe ndiye aliyemtaja huyu mtu anaitwa Mrindoko awajibishwe lakini ripoti ya Richmond imekaliwa. Katika mazingira hayo, kuna kila dalili kwamba uhusiano wa Dk. Mwakyembe na Mwambalaswa ndiyo uliosababisha ripoti ya Richmond isitekelezwe ipasavyo.

“Katika mazingira haya, taifa letu haliwezi kupata mikataba mizuri. Hiki ndicho kilio chetu upinzani, hatuzungumzi mambo madogomadogo, tunazungumza 'issues' (hoja) taifa hili limeuza TRC (Shirila la Reli), ATC (Shirika la Ndege) , migodi, mashamba, Kiwira, Benki ya NBC, mambo yote hayo yamefanywa na serikali yetu ya CCM,”alisema.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia