WAKULIMA wa korosho wamejipatia zaidi ya Sh. bilioni 800 kutokana na kuuza nje ya nchi zao hilo katika msimu wa mauzo uliopita.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Tate ole Nasha, wakati akifungua madhimisho ya Siku ya Korosho, yaliyofanyika kama sehemu ya Maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu J.K Nyerere, Barabara ya Kilwa.
“Serikali imekuja na utaratibu wa kuagiza mbolea kwa mkupuo na pia tutaanza kutoa mbolea kwa bei elekezi. Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha tunawainua wakulima wa korosho na sekta ya kilimo kwa ujumla”, alisema ole Nasha.
Alisema tani 18,000 za mbolea aina ya salfa zitatolewa kwa wakulima bila malipo katika msimu ujao wa korosho hali itakayosaidia kuwaongezea ari wakulima wa korosho, ambao zao hilo lililiingizia taifa fedha nyingi zaidi za kigeni msimu uliopita.
Katika kuwawekea wakulima mazingira wezeshi, ole Nasha alisema Serikali imeondoa zaidi ya tozo 140 zilizokuwa kero kwa wakulima nchini ikiwa sehemu ya mikakati ya kukuza kilimo kwa maendeleo ya viwanda na uzalishaji wa ajira.
“Kukua kwa kilimo kutasaidia kuongeza la ajira kwa vijana wetu wanaohitimu masomo katika vyuo mbalimbali ndiyo maana tunaweka mkazo katika kukuza zao hili ambalo lina faida si za kibiashara tu bali pia katika kujenga afya, ikiwemo kupunguza lehemu mwilini, uzito na kujenga kinga ya mwili”, alisisitiza.
Kwa kuzingatia umuhimu huo, alitoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kula korosho kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watakuwa wanakuza soko la ndani.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Kilimo), Mhandisi Mathew Mtigumwe, kwa upande wake, alisema Siku ya Korosho katika Maonyesho ya Sabasaba ni muhimu kwa kuwa inawakutanisha wadau wa sekta hiyo kwa pamoja.
Pia aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo hali inayoonyesha kuwa sasa kuna mageuzi makubwa katika sekta hiyo.
Bei ya Korosho katika msimu uliopita kwa kilo moja ikikuwa Sh. 4000 hali inayoonyesha kuwa wananchi wakiunga mkono juhudi za Serikali kwa kuzalisha kwa wingi na kuongeza thamani ya zao hilo, hivyo kutoa kutoa mchango mkubwa zaidi katika kujenga uchumi wa viwanda.
