Na. Ahmad Mmow, Lindi.
LICHA ya serikali kupitia mrajisi wa tume ya maendeleo ya ushirika kueleza sababu za kusitisha mikutano mikuu ya kwanza ya vyama vikuu vya ushirika vya Lindi Mwambao na RUNALI. Baadhi ya Wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika wameendelea kuhoji uhalali wa wajumbe wa kamati za muda za vyama vikuu hivyo, ambao sio wajumbe wake wa mikutano mikuu wala wakamati za vyama vyao vya msingi(AMCOS) kuendelea kuwa wajumbe wa kamati hizo.
Wakizungumza na Muungwana kwa nyakati na maeneo tofauti, viongozi na wanachama hao walisema wajumbe wa kamati za muda walioshindwa kuchaguliwa kuwa wajumbe wa mikutano mikuu ya vyama hivyo hawana uhalali wa kuendelea kuwa wajumbe wakamati za muda za vyama vikuu hivyo.Huku Wakiomba serikali kuitisha mikutano mikuu ili nafasi za wajumbe hao ambao wapo kwenye kamati hizo kinyume cha sheria za ushirika ziweze kujazwa.
Mwanachama wa chama cha msingi Nambambo na mjumbe wa mkutano mkuu wa chama cha RUNALI, aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Kassim. Alisema inafahamika kuwa vyama vya msingi vya ushirika vimefanya mikutano mikuu ikiwa ni kutekeleza matakwa ya sheria ya ushirika. Mikutano ambayo imetumika pia kuwachagua viongozi wake na kusoma taarifa za mapato na matumizi ya vyama hivyo.
Alisema sheria inasema viongozi wa vyama vya ushirika watabaki madarakani kwa vipindi vya miaka mitatu. Iwapo wanafaa kuendelea wata chaguliwa tena na wajumbe wa mikutano mikuu ili waongoze kwa muhula mwingine.
" Sasa hao wanamwakilisha nani, tena wanachama wenzao wamekosa imani juu yao, ndio sababu wamewakataa. Lakini pia wamemaliza muhula wao wa uongozi kwa mujibu wa sheria, sasa wanabaki kwenye kamati hizo kwa mujibu ya sheria gani na kwa masilahi ya nani. Hatuna shida na watendaji bali wajumbe. Hao watendaji wanaweza kutumia muda wa matazamio kujiendeleza kielimu," alifafanua na kuhoji Rashid.
Alisema kutokuwa na usajili kamili sio sababu ya kuvunjwa sheria ambayo imewekwa ili kukidhi matakwa ya demokrasi kwenye vyama vya ushirika. Hivyo sababu hiyo inalengo la kuminya demokrasi na kuongozwa na watu wasio na sifa.
Mjumbe huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa serikali wajibu wake ni kuvilea vyama na kuvipa miongozo, taratibu na sheria za ushirika. Bali vyama hivyo ni mali ya Wanachama, nandio wenye haki ya kuwaondoa na kuwaweka viongozi wake kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Mwanachama Mohamed Mtopoka wa New Matekwe AMCOS, alisema kukosekana kwa uhalali wa wajumbe wa kamati za muda za vyama vikuu hivyo ambao sio wajumbe wa mikutano mikuu yake ni jambo lililowazi. Bali kinachofanyika nikuwekewa viongozi wa sio na ridhaa nao.
Mtopoka alisema wanachama wa vyama vya msingi wanajua mwenendo na tabia za wajumbe wa kamati ambao hawakuchaguliwa kwenye mikutano mikuu ya vyama vyao vya msingi. Kwahiyo ni kitendo kisichokubalika waongoze vyama vikuu ambavyo wanachama wake ni vyama vya msingi.
Mwenyekiti wa chama cha msingi NANYUM , Hassan Hamisi, licha ya kuiomba serikali isikilize maoni ya wadau kuhusu usitishaji wa mikutano hiyo, alisema itakuwa ni kitendo cha aibu kwao kukubali kuongozwa na viongozi wasiochaguliwa na wanachama, wakati wao walichaguliwa na wanachama kwenye mikutano mikuu ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.
"Sisi waliotuchagua wanatuamini, ndio sababu wanatukabidhi mazao yao tukawauzie . Halafu sisi tuwakabidhi watu ambao hata vyama vyao vya msingi vimeshindwa kuwaamini, nijambo lisilowezekana. Labda tulazimishwe, "alisema Hassan.
Mmoja wa wakulima wanaovuna kwa wingi zao la korosho wilayani Nachingwea, ambae hakutaka jina lake liandikwe, kwa madai kuwa anaogopa kusakamwa na vigogo wenye mamlaka,bila kuwataja yao na mamlaka alisema nijambo lisilokubalika kuona viongozi walioondolewa kupitia chombo cha serikali yenyewe, COWASCO kwenye vyama vyao vya msingi wanaendelea kuwa wajumbe wa kamati za muda za vyama hivyo. "Ujue sisi tunayajua mengi kuhusu hao watu kuliko wanavyo wajua wao. Lakini tukisema kweli tutaanza kutishana na kuitana majina mabaya, waiche demokrasi ifanye kazi hata kwenye vyama ushirika ili kuepusha migogoro," alisema.
Mrajisi msaidizi wa tume ya maendeleo ya ushirika wa mkoa wa Lindi, Benjamin Mwangwala, alisema mchakato wa uchaguzi wa vya vikuu hivyo ulisitishwa kwa mujibu wa sheria ya ushirika namba 6 ya mwaka 2013, kifungu cha 41 ambacho kinaeleza wazi kwamba chama kikishaandikishwa kinatakiwa kufanya mikutano ya awali (ya kwanza) ambavyo vimepewa usajili wa muda. Ambapo vimepewa muda wa miaka miwili kwa ajili ya matazamio ili viweze kutekeleza na kukidhi matakwa ya kisheria.Kabla ya kupewa usajili wa kudumu.
" Nikweli vilitaka kufanya mikutano hiyo tarehe 14 na 17, mwezi Julai mwaka huu, hata hivyo mrajisi kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria alisitisha mikutano hiyo. Nikwasababu havija kidhi vigezo vya kuweza kufanya mikutano hiyo kwa mujibu wa sheria ya ushirika namba 36 ya mwaka 2013, "alisema Mwangwala.
Aliyataja baadhi ya mambo ambayo vyama hivyo vinatakiwa kufanya kuwa nipamoja na kuwasilisha taarifa za ukaguzi kuhusu wanachama wake (AMCOS), kuwasilisha taarifa itakayo onesha mtiririko wa mwenendo wa wanachama waanzilishi wa vyama hivyo,ambayo itabainisha wazi nia ya kuanzisha vyama hivyo.Ili kuonesha na kuthibitisha kuwa wanachama wake sio wanachama wa vyama vikuu vingine vya ushirika.
Jambo jingine ni kukamilisha mchakato wa kufilisi chama kikuu cha Ilulu ambacho mpaka sasa kinatambulika kwenye usajili. Lakini wanachama wake ni hao hao waliopo kwenye vyama vikuu vya Lindi Mwambao na RUNALI.
Alisema usajili wa vyama vya Lindi Mwambao na RUNALI ulifanyika kwa mujibu wa kifungu cha 32, ibara ya 21. Na kuonesha wazi kuwa kamati hizo ni za muda tu. Kwasababu vyama hivyo havijapata usajili wa kudumu.
Hivi karibuni serikali kupitia mrajisi wa tume ya maendeleo ya ushirika, Tito Haule ilitoa ufafanuzi kuhusu kusitishwa mikutano mikuu hiyo, sababu na hatima ya wajumbe wa kamati za muda za vyama vikuu hivyo ambao sio wajumbe wa bodi wa vyama vyao msingi wala mikutano mikuu ya vyama vikuu .
Kuhusu wajumbe wakamati hizo, alisema kwamba haikuwa na sio lazima wajumbe wake wawe ni wajumbe wa bodi za vyama vyao vya msingi. Bali uanachama wao unawezesha kuwa wajumbe wa kamati hizo za muda.Iwapo hawakabiliwi natuhuma za kutokuwa waaminifu na nyingine zilizo kinyume na maadili mema ya kiongozi.
