Mchungaji Msigwa, Ridhiwani Kikwete vuta nikuvute Bungeni

By Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz
Dodoma. Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa jana walirushiana maneno kila mmoja akionyesha umahiri wa kutunga sheria.

Hayo yalijitokeza wakati Bunge lilipoketi kama kamati chini ya mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga kupitia vifungu vya muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa 2017.

Muswada huo ambao ulichangiwa na wabunge wawili tu, mmoja wa CCM na mwingine kutoka kambi ya upinzani uliwasilishwa bungeni na mwanasheria mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya mbunge wa viti maalumu (Chadema), Ruth Mollel kushikilia msimamo wa kuwapo usawa wa kijinsia katika muundo wa bodi ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.

Katika muswada huo, Masaju alipendekeza bodi hiyo iwe na wajumbe tisa wakiwamo wawakilishi wawili wawili wanaowakilisha vyama vya waajiri vyenye wanachama wengi kwenye mfuko huo.

Pia alipendekeza wajumbe wawili wawili wanaowakilisha vyama vya wafanyakazi vyenye wanachama wengi kwenye mfuko na wakili wa Serikali kuanzia ngazi ya mwandamizi atakayemwakilisha AG.

Wajumbe wengine ni mwakilishi wa wizara yenye dhamana ya hifadhi ya jamii, mwakilishi wa Wizara ya Fedha, mwakilishi wizara inayoshughulikia utumishi wa umma na wa jumuiya ya watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, Mollel aliwasilisha jedwali la marekebisho akipendekeza muundo huo uzingatie jinsi ya kike badala ya kuliacha suala hilo katika utashi wa mtu mmoja ambaye atakuwa anateua.

Pamoja na Masaju kueleza madhara ya kuingiza kifungu cha aina hiyo katika sheria, bado mbunge huyo alisimama katika msimamo wake na kutoa hoja kuwa Bunge lijadili suala hilo.

Ndipo mwenyekiti alipomruhusu Ridhiwani kuchangia na aliposimama alisema yeye amesimama si kuunga mkono hoja ya Mollel, bali kutoa maoni kuhusiana na uandishi wa sheria.

“Sina hakika sana kama mama yangu (Ruth) ni mwanasheria. Katika uandishi wa sheria nchi hii hakuna sheria inayoandikwa kwa kuzingatia gender (jinsi). Hilo la kwanza tuelewane,” alisema.

“Unapoweka kipengele chochote kile kwamba iwe kipengele hiki kimzungumzie mtu huyu awe mwanamme ni tayari kuna mtu (mwanamke) umeshambagua.

“Unaposema kipengele hiki kiwe mwanamke maana yake kuna watu tayari umeshawatenga. Kinachotakiwa ni busara ya wale wanaoteua si jambo la kuandika gender.”

Hata hivyo, Mchungaji Msigwa alipopewa fursa alisema itakuwa ni makosa makubwa kutoingiza kipengele hicho na kurudi nyuma kwenye historia ya jinsi mwanamke alivyofanywa kama “object”.

“Ni wakati sasa hivi wa wanawake kuamka ili kuhakikisha mnatetea haki zenu ili tufikie kiwango kile cha 50-50 hata tunapotunga sheria. Mfano mzuri ni ile sheria inayomlazimisha Rais kuteua wabunge, ” alisema mbunge huyo.

Aliongeza kuwa sheria hiyo inamlazimisha Rais kuteua angalau nusu ya wabunge wawe wanawake na kuna wakati Rais John Magufuli aliteua wabunge wengi wanaume.

Hali ndani ya ukumbi wa Bunge ilikuwa kama ifuatavyo:

Ridhiwani: Mwenyekiti taarifa.

Msigwa: Hatutoagi taarifa kwenye kuchangia.

Ridhiwani: Leo ndio unapewa taarifa hapa leo. Wanataka kutuyumbisha bwana. Hatuwezi kuyumbishwa bwana sisi tunatengeneza sheria.

Msigwa: Hata mimi natengeneza sheria.

Ridhiwani: Hakuna namna hiyo Msigwa bwana. Hatuwezi kutunga sheria ambazo ziko biased (zina pendelea).

Mwenyekiti wa Bunge: Waheshimiwa wabunge. Naomba mkae nyinyi nyote wawili maomba mkae wote wawili. Mheshimiwa AG tuendelee.

Ridhiwani: Sie tumesoma sheria bwana.

Mwenyekiti wa Bunge: Mheshimiwa Stella Manyanya (Naibu Waziri wa Elimu).

Stella Manyanya: Kwanza nataka kumuambia bwana Msigwa. Si vyema kutumia vibaya kumtaja mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo sio lazima sana. Kwa mfano kumwambia alimuondoa mbunge.

Naibu waziri huyo alimtaka Mchungaji Msigwa asipitilize katika suala hilo akisema kama mbunge alijiuzulu mwenyewe ni vyema akasema hivyo, kuliko kusema Rais ndiye aliyemuondoa.

Hata hivyo Masaju alipopewa kuchangia mjadala huo alianza kwa kusema, “namshukuru sana mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ametusaidia kuweka suala hili vizuri. Ukirudi kwenye uandishi wa sheria. Tunayo sheria ya kwanza kabisa inayoitwa sheria ya tafsiri ya sheria. Yenyewe ndio msingi wa tafsiri ya sheria zote na ndio muongozo wa kutafsiri sheria.”

“Mbona kwenye sheria inasema He (mwanamme) lakini wanawake wamo humo ndani. Tunao muongozo mahsusi unaotuongoza katika kuandika sheria.”

Mollel alipopewa fursa ya kuhitimisha hoja yake alisema amesikitishwa na jinsi hoja hiyo ilivyochukuliwa akisema yeye akiwepo serikalini waliweka utaratibu wa usawa kwa wote.

Mwenyekiti wa Bunge aliamua suala hilo liamuliwe kwa kura, ambapo baada ya kuwahoji wanaoafiki juu ya hoja ya mbunge huyo waseme “Ndioo” na wasioafiki waseme “Sioo”, waliosema “Sioo” walishinda.

Muswada huo ulipitishwa na Bunge kuwa sheria na sasa unasubiri sahihi ya Rais Magufuli ianze kutumika.
 
Mpya zaidi Nzee zaidi