Shambulizi lililoua askari 15 wa JWTZ UN yaainisha kasoro


Dar es Salaam. Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kushambuliwa na kuuawa askari 15 wa Tanzania walioko katika operesheni ya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imebanisha kasoro kadhaa ikiwamo kukosekana mpango kazi wa kusaidia uokoaji.

Ripoti hiyo iliyotayarishwa na wataalamu waliochaguliwa na katibu mkuu wa UN, Antonio Guterres imesema kutokuwapo mkakati wa dharura kulisababisha Tanzania kupoteza askari wengi.

“Katika uchunguzi wetu tumebaini upungufu mkubwa, mojawapo ni kwamba vikosi vya kulinda amani nchini Congo havina mpango kazi wa dharura kwa ajili ya kuongeza nguvu na kuokoa askari wakati kunapojitokeza tukio la uvamizi,” inasema ripoti hiyo iliyotayarishwa na wataalamu wa masuala ya ulinzi, siasa na usafirishaji wakiwamo maofisa wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Tanzania ilipoteza askari 15 wakati wapiganaji wa kundi la ADF walipovamia moja ya vituo vya askari wa kulinda amani katika eneo la Beni, Kivu Kaskazini.

Mashambulizi hayo yaliyotokea Desemba 7, 2017, pia yalisababisha askari wengine 43 kujeruhiwa na mmoja hakujulikana alipo, Askari 14 waliuawa katika eneo la tukio huku mwingine akifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Hilo ndilo shambulizi kubwa zaidi kutokea kwa vikosi vya Tanzania tangu vianze kushiriki operesheni za amani duniani.

Katika ripoti hiyo, wataalamu hao wamebainisha kuwa kukosekana kwa usimamizi na vitendea kazi kulichangia shambulizi hilo kufanyika.

“Kutokuwapo mwongozo wa kiutendaji ni moja ya eneo lililobainika lakini kuna mambo mengine kama vile kukosekana kwa vyombo vya anga, wahandisi na intelijensia. Haya ni masuala ambayo yanapaswa kushughulikiwa haraka,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema licha ya wapiganaji wa ADF kuendelea kutumia mfumo wa aina moja katika mashambulizi mengine mawili ya awali, kulikuwa hakuna kizuizi walichokuta hivyo kuthibitisha hoja kuwa vikosi vya UN havikujipanga ipasavyo.

Ndani ya ripoti hiyo, wataalamu wameshauri ofisi ya Monusco, UN na nchi zinazochangia vikosi vya kulinda amani kuwa zinapaswa kuanzisha mkakati wa pamoja ili kuviwezesha vikosi hivyo kuchukua jukumu la kushambulia waasi na hasa katika maeneo yanayotazamwa kuwa na mazingira magumu.

Wataalamu hao wametaka kuwapo kwa utashi wa kisiasa katika eneo la ukanda huu ili kusaidia kutoa picha halisi kuhusu hatari ya kiusalama inayoendelea kusababishwa na ADF.

Kauli ya Serikali
Akizungumzia ripoti ya UN, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi alisema wanatambua uwepo wake lakini bado haijafikishwa rasmi serikalini.

“Bado sijaiona ripoti hiyo, hivyo nitahitaji niipate kisha niisome ndipo Serikali itatoa maelezo yake,” alisema Dk Mwinyi alipozungumza na Mwananchi.

Alisema mbali na ripoti ya UN, Tanzania iliunda timu ya wataalamu wake wa ndani kuchunguza shambulizi hilo.

“Tangu tuwape kazi hiyo nadhani hadi sasa watakuwa wamekamilisha uchunguzi wao. Nasubiri nione ripoti zote mbili kisha tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa maelezo zaidi,” alisema.

Mbali ya Congo, Tanzania imewahi kukumbwa na mkasa wa kupoteza askari wake katika Jimbo la Darfur nchini Sudan.

Tanzania imekuwa ikishiriki katika operesheni za kulinda amani katika sehemu mbalimbali duniani na imewahi pia kutuma askari Liberia na Lebanon.

Mpya zaidi Nzee zaidi