Serikali imeimarisha ulinzi na usalama kwa watu wenye ualbino

Na James Timber, Mwanza

Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli imeimarisha ulinzi na usalama kwa watu wenye ualbino  kwani uwepo wao ni mchango tosha wa maendeleo na ukuaji wa uchumi katika jamii.
Akizungumza hayo katika uzinduzi wa Mradi Jumuishi wa Watu wenye ualbino na warsha ya kuhamasisha kulinda na kutetea haki za watu wenye ualbino Mkuu wa Wilaya Misungwi mkoani Mwanza Juma Sweda alisema Jeshi la Polisi lipo makini kuhakikisha watu hao wanaishi kwa amani bila hofu.

"Watu wenye ualbino wamekuwa salama sababu jeshi la polisi liko makini na linafanya kazi bila kubahatisha ambapo hadi sasa tunamshikilia kijana mmoja kwa kupanga mauaji ya watu wenye ualbino ambapo alitaja mtandao wake wote," alisema Sweda.

Mwenyekiti wa Tanzania Albinism Society (TAS) Misungwi Charya Saguja, alisema baadhi ya changamoto zinazowakabiri ni kuishi katika kambi bila kujishughulisha jambo inalowafanya wajihisi wametengwa, suala linalopelekea wengi wao wanakuwa omba omba mtaani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi alimwagiza Afisa Ustawi wa Jamii kusimamia vikundi vitakavyoanzishwa na TAS kwa ajili ya kupewa mikopo itakayo wainua kiuchumi.

Naye Meneja Mradi wa watu wenye ualbino Florence  Rugemalira alieleza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali  imewezesha kupungua kwa vitendo vya mauaji, ukatwaji viungo na kutishiwa kwa watu wenye ualbino.

Aidha mmoja kati ya washiriki wa semina hiyo Zainabu Abdalah alifurahishwa na mradi huo kwa kuwatambua ambapo ameiomba mamlaka husika kupunguza idadi ya watu wenye ualbino katika makao ya muda na kuunganishwa kwenye familia zao kama zamani.

Mpya zaidi Nzee zaidi