Matumizi ya VAR yakutana na kigingi EPL

Vilabu vya England vinavyoshiriki ligi kuu ya soka nchini humo EPL vimepiga kura ya kukataa kuanza kwa matumizi ya Video Assistance Referee (VAR) kwa msimu wa 2018/19 katika ligi hiyo.

Vilabu hivyo vimekubaliana kuendelea kufanya majaribio kwa teknolojia hiyo kwa msimu mwingine kabla ya kuamua vinginevyo haswa baada ya kuwa na kasoro kadhaa ambazo zinafanya teknolojia hiyo isiaminike.

Aidha timu hizo zimekosoa baadhi ya makosa ambayo yamekuwa yakifanya na waendeshaji wa vymbo vya teknolojia hiyo ikiwemo mistari inayoonekana kwenye Video wakati wa matukio kama ya 'offside' kutokuwa imenyooka.

Badala ya kuanza msimu ujao vilabu hivyo vimependekeza Teknolojia hiyo iendelee kufanyiwa majaribio kwenye michuano kama Kombe la ligi EFL na Kombe la FA ili wajiridhishe kama makosa kama hayo yamefanyiwa marekebisho.

Kwa upande mwingine ligi ya Ujerumani imeanza matumizi ya teknolojia hiyo msimu huu huku La Liga wao wakijipanga kuanza kutumia VAR kwa msimu wa 2018/19. FIFA pia imeshathibitisha kuwa VAR itatumika kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.


Mpya zaidi Nzee zaidi