Baada ya kuwepo na malalamiko ya kunyimwa kwa mke wa Mfanyabiashara , Harbinder Singh Seth, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa ruhusa mfanyabiashara huyo kutembelewa na mke wake gerezani.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Shahidi, baada ya Wakili wa Seth, Dora Maraba kuiomba mahakama kibali kwa ajili ya mke wa Seth, kwenda kumuona mumewe gerezani.
Wakati akiomba kibali hicho Maraba alimwambia Hakimu kuwa "Tuliandika barua kwa mkuu wa Gereza la Ukonga, tukiomba mke wa Seth, aweze kuruhusiwa kumuona mumewe lakini imeshindikana, hivyo tunaomba Mahakama yako, itupatie kibali ili Seth aweze kuonana na mke wake,".
Amesema "Mwezi uliopita, mke wa Seth alifiwa na mama yake mzazi, hivyo tangu kutokee kwa msiba huo, mkewe hajapata nafasi ya kuonana na mume wake, gerezani"
Aidha baada ya Hakimu Shahidi, kusikiliza maelezo ya pande zote, amesema mshtakiwa ana haki ya kupewa nafasi ya kuonana na kuongea na mke wake kwa sababu bado hajatiwa hatiani.
“Japokuwa hatupaswi kuingilia taratibu za magereza, lakini mshtakiwa ana haki ya kupewa nafasi ya kuongea na mke wake, hivyo naomba aruhusiwe kuongea na mke wake," Hakimu Shahidi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 21, 2018, itakapotajwa tena.
Wafanyabiashara Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi.
Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.
