Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haiwezi kumbadilisha msimamizi wa uchaguzi mdogo wa marudio wa jimbo la Buyungu kwa kuwa chama cha CHADEMA hawakufuata taratibu za kisheria za kumkataa msimamizi huyo.
Ufafanuzi huo umetolewa leo Agosti 08, 2018 na Mkurugenzi wa Tume hiyo Dkt. Athumani Kihamia na kusema kwamba mujibu wa Kifungu cha 7 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, malalamiko yaliyotolewa hayana msingi wa kisheria kwa sababu haya kwenda kama rufaa ila yametolewa kama malalamiko.
"Napenda kuwajulisha umma kwamba malalamiko hayo hayawezi kumuondolea sifa msimamizi wa uchaguzi kwa kumuondoa kusimamia shughuli za uchaguzi katika Jimbo la Buyungu. Kwa kuwa CHADEMA imelalamika kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na malalamiko hayo wameyaleta kama barua, malalamiko hayo yalipaswa yaletwe ndani ya muda unaokubalika ambayo ni saa 48 tangu kupokea hizo taarifa", amesema Dkt. Kihamia.
Mbali na hilo, Dkt. Kihamia amekiasa chama cha CHADEMA kuwa kama kuna kasoro zingine zozote ndogo ndogo ambazo zinaweza kutatulika kwa njia ya kawaida Tume itatekeleza
majukumu yake katika kasoro hizo.
Dkt. Kihamia amebainisha hayo baada ya CHADEMA kuiandikia barua Tume hiyo na kuilalamikia juu ya msimazi wa uchaguzi kushindwa kutoa ratiba ya mtiririko wa uchaguzi, kushindwa kutoa orodha ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura pamoja na kushindwa kuonesha sehemu ambapo kura zinatakiwa kujumlishwa.
Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Buyungu na kata 77 unatarajiwa kufanyika Agosti 12, 2018, baada ya jimbo hilo kuwepo wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Kasuku Samson Bilago aliyefariki Mei 26 mwaka huu na kupelekea jimbo hilo kuwa wazi hadi sasa.
Mtazame hapa chini Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Athumani Kihamia akiongea zaidi juu ya jambo hilo.
