SERIKALI kupitia Wizara ya Uvuvi na Mifugo imezindua mkakati wa kudhibiti magonjwa ya mifugo, ambao utaboresha usimamizi wa sheria na kanuni za uchanjaji na uogeshaji.
Hatua hiyo imelenga kulinda mifugo hiyo dhidi ya magonjwa mbalimbali na kusaidia wafugaji kuzalisha mifugo yenye afya bora, itakayokidhi vigezo katika soko la kimataifa.
Uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha Chamakweza, Halmashauri ya mji wa Chalinze mkoani Pwani ulioambatana na uogeshaji mifugo kwa ajili ya kuwakinga na magonjwa.
Waziri Mpina alisema mpango huo umelenga kuboresha sekta ya mifugo ili kuhakikisha hakuna magonjwa nchini.
Alieleza kuwa maamuzi ya kuanzisha mpango huo yanatokana na mifugo mingi nchini kukabiliwa na magonjwa na kuathiri soko la sekta hiyo.
Mkakati huo pia utasaidia kuimarisha sekta hiyo na nchi kuwa na mifugo salama itakayouzwa katika soko la kimataifa.
Alisema kwa sasa serikali ya awamu ya tano, imejipanga kupambana na magonjwa ya mifugo inayopatikana nchini.
Hata hivyo, alisema mkakati huo umepangwa kusambazwa nchi nzima hasa katika maeneo ambayo yamekuwa na wafugaji lengo likiwa ni kuhakikisha magonjwa yote yanayotokana na mifugo yanadhibitiwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka wizara hiyo, Dk. Martin Ruhete, alisema mpango huo utaenda kuhuisha na kuboresha sheria zinazosimamia masuala ya uchanjaji na uogeshaji.
Alisema mpango huo utahusisha mifugo yote kwa kupanga ratiba ya uogeshaji na uchanjaji nchi nzima.
Kutokana na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa dawa za chanjo za mifugo, alisema mkakati huo utakuja na mpango utakaowezesha kupatikana kwa dawa hizo ambazo zitatumika kwa wakati mmoja na kwa bei nafuu lengo likiwa ni kukomesha magonjwa ya mifugo.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji, Katibu wa chama cha wafugaji Tanzania, Maghembe Makoye, alisema wanaupokea mpango huo na wanadhani utasaidia kutatua changamoto kwa wafugaji wengi ambao walikuwa wakishindwa kukabiliana na magonjwa hayo.
Alisema changamoto nyingine iliyokuwa ikiwaumiza ni ya magonjwa yanayoikabili sekta hiyo.
