TFF, wadhamini Ligi Kuu Bara wajifungia

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema bado wapo kwenye meza ya mazungumzo na Kampuni ya Vodacom kuhusu kusaini mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini akaeleza kuwapo kwa uwezekano wa kuongezeka wadhamini wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Bin Zubeiry Sports - Online, Karia ameeleza kushangazwa na wanaodai kuanzia msimu ujao Ligi Kuu haitakuwa na mdhamini mkuu.

“Inafahamika kila mkataba wa Vodacom unapofikia tamati, mazungumzo huwa mazito na ya mvutano hadi makubaliano yanafikiwa dakika za mwisho kabla ya Ligi Kuu kuanza, watu wavute subira, bado tunaendelea na mazungumzo,”Karia alinukuliwa.

Pamoja na hayo, Karia ameeleza kuna uwezekano Ligi Kuu ikawa na wadhamini zaidi ya wawili msimu huu, kwani mazungumzo na kampuni mbalimbali yanaendelea vizuri.

Ligi Kuu msimu wa 2018/19 inatarajiwa kuanza Agosti 22, mwaka huu na hadi sasa ni Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) tu wamesaini mkataba mpya wenye thamani ya Sh. milioni 420, huku wasiwasi ukiwa ni juu ya wadhamini wakuu, Vodacom.

Ligi Kuu itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya mabingwa watetezi, Simba dhidi ya washindi wa Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC), Mtibwa Sugar ambao utapigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Agosti 18.

Mahasimu wa jadi, Simba na Yanga watakutana Septemba 30, mwaka huu katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara

Ligi hiyo msimu huu inajumuisha timu 20 tofauti na msimu uliopita ambao ulikuwa na timu 16.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia