Na James Timber, Mwanza
Watu watatu Wakazi wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa kosa la kujihusisha na shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali na kutumia vifaa vinavyotumika kupigia ramli chonganishi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni mwanamke mmoja Mariam Ramadhan na wanaume wawili ambao ni John Luzaria na Masanja Majige wote ni Wakazi wa Misungwi.
"Tumewakamata hawa kutokana na kupata ushirikiano kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu wanafanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali, ndipo askari wetu waliopo doria walifuatilia kwa haraka na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na vifaa vinavyotumika kupigia ramli chonganishi," amesema Kamanda Msangi.
Aidha Kamanda Msangi ameeleza kuwa watuhumiwa wote watatu wapo katika mahojiano na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka, huku akitoa rai kwa watu wanajihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja kwani wanakwamisha maendeleo.
