Na James Timber, Mwanza
Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu (SUMATRA) imetoa tahadhari kwa watumishi wa mamlaka hiyo wanajihusisha na utoaji wa leseni bandia kwa wadau wa usafirishaji kwa njia ya barabara hawatasalimika kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria haraka.
Akizungumza na Wadau wa Usafirishaji kwa njia ya Barabara katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa jijini Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA Gilliad Ngewe, amesema kuwa anawaomba wadau wenye leseni ambazo hazijahakikiwa wakahakiki mapema katika mfumo mpya wa maombi ya Leseni kwa njia ya mtandao ili kuleta ufanisi zaidi.
"Wadau wa Usafirishaji naomba muepukane na vishoka na mtupe ushirikiano ili kuwabaini wenye mtandao unaojihusisha na utengenezaji, wa leseni zisizohitajika, kwani wanadhorotesha huduma itolewayo na mamlaka yetu," alisema.
Aidha Mkurugenzi amesema kuwa wanaoruhusiwa kukata leseni ni mmiliki wa chombo na siyo dereva, ambapo katika kukagua kwa ufanisi kama leseni imemfikia mlengwa mamlaka itakuwa inatoa taarifa za mara kwa mara.
Meneja Leseni na Ukaguzi SUMATRA Leo Ngowi amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kwa njia ya barabara kufanya maombi kwa njia ya mtandao huku akibainisha faida zake ni kupunguza muda, kujua kosa la gari lako, kuokoa gharama za usafiri na kutunza kumbukumbu kwa uhakika.
Mwenyekiti Msaidizi wa Chama Cha Madereva wa Daladala jijini hapa (MWAREDA) Ezekiel Lameck amewaomba SUMATRA kuboresha sheria ili kumpa haki mlemavu kutokana na wengi wao kutokutumia usafiri wa daladala wakiogopa miundombinu siyo rafiki.
