Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hivi karibuni inatarajia kuwafanyia upasuaji Wagonjwa 20 wa Moyo wa kufungua kifua na kuwekewa valvu zaidi ya mbili (milango ya moyo) kwenye kambi maalum ya matibabu itakayofanyika katika Taasisi hiyo.
Upasuaji huo unafanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya Saudi Arabia.
Dk. Bashir Nyangasa, ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, alisema hayo jana wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Dk. Nyangasa pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu alisema upasuaji huo unafanywa kwa wagonjwa ambao valvu zao tatu hazifanyi kazi vizuri, zinabadilishwa na kuwekwa za bandia.
“Kambi hii ni ya siku saba tangu ilipoanza tumefanya upasuaji na kubadilisha valvu kwa wagonjwa tisa ambao hali zao zinaendelea vizuri na hii leo (jana) wataanza kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kurudi wodini kuendelea na matibabu,” alisema Dk. Nyangasa.
Kwa upande wa uhitaji wa damu wakati wa upasuaji, Dk. Nyangasa alisema mgonjwa mmoja anatumia kati ya chupa tano hadi saba, lakini kama mgonjwa atapata tatizo anaweza kutumia chupa zaidi ya hizo na kuwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu.
Aidha, Dk. Nyangasa aliwasisitiza wananchi kujiunga na mifuko ya bima za afya wakiwa bado na afya njema badala ya kusubiri kujiunga wakati wakiwa wagonjwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) Tanzania, Hassan Katungunya alisema wanashukuru wataalamu hao kuja hapa nchini kufanya matibabu ya moyo kwa wagonjwa.
“Ni faraja kuona miongoni mwa Watanzania wanyonge wanapata msaada wa matibabu kwa kuwa upasuaji wa moyo ni wa gharama na kuna wengine hawana uwezo wa kulipa.”
“Tunaomba uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia uendelee. Wageni wetu hawa wamepata faraja kwa kuona nchi yetu inawajali na hawapati usumbufu wakati wa kuingia na kutoka nchini,” alisema.
Wataalamu wa afya 15 wamekuja kwa ajili ya kufanya upasuaji wa moyo, kati ya hao kuna madaktari bingwa, madaktari wa usingizi na wagonjwa mahututi, wataalamu wa mashine za moyo na wauguzi.
