KOCHA MKUU WA TIMU YA SOKA YA UGANDA (CRANES), MFARANSA SEBASTIEN DESABRE.
Cranes imelazimishwa sare ya bila kufungana na Taifa Stars katika mechi ya Kundi L ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 zitakazofanyika Cameroon mwakani.
Desabre alisema timu yake ilishindwa kutumia vema nafasi mbili za wazi walizotengeneza katika kipindi cha kwanza na kueleza kwamba walikuwa katika kiwango bora kwenye dakika 25 za kwanza tu.
Mfaransa huyo alisema pia kipindi cha pili waliingia wakiwa na mbinu tofauti, lakini hawakuweza kupata nafasi ya kufunga na kujiweka katika nafasi ngumu ya kampeni hizo za kucheza fainali za AFCON hapo mwakani.
"Kiufundi kipindi cha pili hatukua vizuri, nasema matokeo yameniumiza, ili tufuzu tunahitaji kuwa na pointi 10, tunahitaji kushinda mechi mbili kati ya nne zilizobakia, ila naamini tunaweza kuzipata na kusonga mbele katika hatua inayofuata," alisema kocha huyo.
Hata hivyo, kocha huyo alisema hakuwa na muda mrefu wa kukiandaa kikosi hicho kutokana na majukumu waliyokuwa nayo sehemu kubwa ya wachezaji wake wanaocheza nje ya Uganda.
"Hiki kilichoonekana kimetokana na kufanya mazoezi kwa siku saba tu, mwezi ujao tutakuwa na mechi mbili, tunahitaji kushinda tu, Tanzania wana timu nzuri, ukimwangalia Samatta (Mbwana), Msuva (Simon), utaona wana timu ya aina gani," aliongeza Mfaransa huyo.
Nahodha na kipa wa Cranes, Denis Onyango, alisema mechi hiyo ilikuwa ngumu, lakini uzoefu wao na hasa yeye umesaidia kupata matokeo hayo ya sare ambayo hawajayafurahia.
"Haikuwa mechi rahisi, ni "dabi" ya Afrika Mashariki sasa, tunahitaji pointi sita ili tuweze kufuzu, Tanzania ndio wapinzani wetu kwa sasa na si Kenya, tutafanya bidii zaidi ili tufikie malengo yetu, timu ina ari na morali kubwa ya kuhakikisha hatupotezi tena pointi," alisema kipa huyo anayecheza katika klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Onyango alisema alitumia uzoefu na kuonyesha ubora wake kudaka shambulizi la hatari lililofanywa na Samatta na hapo alidhihirisha ukongwe wake.
