Serikali yafunguka kushuka kwa gharama za kumtunza Faru Fausta


SERIKALI imesema gharama za kumhudumia faru Fausta (53) zimeshuka kutoka Sh. 1, 445, 571 hadi Sh. Sh. 285,000 kwa mwezi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, alisema hayo jana bungeni mjini hapa alipokuwa akijibu swali la Mbunge waViti Maalum (Chadema), Suzan Mgonokulima.

Katika swali lake, mbunge huyo alisema serikali inamhudumia faru huyo kwa gharama ya Sh. milioni 64 kwa mwezi ambaye hazalishi kutokana na kuwa mzee sana.

"Lakini serikali hiyo haiwezi kumhudumia mwananchi aliyezeeka ambaye hawezi kufanya shughuli zozote za kujikimu maisha na hana mtu wa kumsaidia. Je, ni kipi kilicho muhimu zaidi kwa serikali kati ya faru Fausta au mwananchi mzee asiyeweza kufanya lolote na hana wa kumsaidia?" Alihoji.

Akijibu swali hilo, Hasunga alisema faru huyo amekuwapo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro tangu mwaka 1965 na kwa sasa ndiye mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani.

"Kutokana na uadimu wa wanyama hao, uwepo wa faru Fausta umekuwa kivutio kikubwa kwa watalii na watafiti wa ndani na nje ya nchi, hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato katika Hifadhi ya Ngorongoro na serikali kwa ujumla," alisema.

Kutokana na uzee, alisema faru huyo alijeruhiwa na fisi Septemba 4, 2016, hivyo kulazimu atunzwe kwenye kizimba kwa ajili ya uangalizi maalum ambao unahusisha matibabu, chakula na ulinzi.

"Gharama kubwa iliyokuwapo kipindi kilichopita ilitokana na hali ya dharura iliyohitajika ikiwamo miundombinu, ulinzi, matibabu na malisho maalumu ambayo matumizi kwa mwezi yalikuwa Sh. 1,445,571," alisema.

Naibu Waziri alisema kwa sasa afya ya faru huyo inazidi kuimarika kadri siku zinavyozidi kwenda, hivyo gharama ya uangalizi imeshuka hadi Sh.285,000 kwa mwezi.

Hata hivyo, alisema faru huyo si kwamba ni muhimu kuliko binadamu wazee bali uamuzi wa kumtunza kwenye kizimba ulifanyika kwa lengo la kunusuru maisha yake, ili hatimaye aendelee kuwa kivutio cha utalii na kuingiza fedha za kigeni nchini.

"Fedha zote hizi zinaingia kwenye mfuko mkuu wa serikali," alisema.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alihoji utunzwaji wa faru Fausta umewezesha kulitumikisha taifa kwa gharama kubwa kuliko wazee Watanzania waliofanya kazi ya kuleta haki na amani katika taifa hadi faru huyo kuonekana ni wa muhimu kwa ajili ya amani iliyopatikana kwa wazee hao.

"Je, serikali haioni ni wakati sasa wa kuhakikisha wazee wa taifa hiliwanatunzwa kama vile gharama zilizotumika kwa faru Fausta ili waweze kuleta amani katika nchi?" Alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Hasunga alisema kwamba wanyama wana haki sawa kama binadamu wengine, na huyo mnyama kutokana na umuhimu wake na ni mmoja kati ya wanyama walio hatarini kutoweka ndio maana amewekwa kwenyeulinzi maalum.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia