MWENYEKITI MTENDAJI WA IPP, DK. REGINALD MENGI.
Dk. Mengi aliyasema hayo juzi wakati wa hafla ya maadhimisho ya benki hiyo iliyotimiza miaka 10 tangu kuanza kwake.
Dk. Mengi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliwaeleza kuwa kutokana na mabadiliko, benki zinatakiwa kuwa wabunifu, wakarimu kwa wateja wao wanaowahudumia kila siku.
Pia aliitaka benki hiyo iwekeze zaidi katika teknolojia, ili kuwalinda wateja wake na vitendo vya wizi wa mitandao.
"Mhakikishe kila mnapotoa huduma wateja wenu wanazifurahia, uaminifu ni jambo la muhimu katika huduma mnazotoa lazima muwaridhishe wateja, kujitoa kwenu kwa wateja mtajifunza mengi na uaminifu ni jambo muhimu.
"Kuna watu wanakwenda benki fulani kwa sababu tu ya huduma nzuri anayopata kutoka kwa watoa huduma, wanakutana na watu wakarimu, mnapoajiri mnatakiwa muajiri watu wenye ukarimu ambao watawahudumia wateja wenu vizuri," alisema.
Kadhalika alisema wanaposema wanaweza akili hufanya kazi, lakini wanaposema hawawezi watakuwa hawawezi kweli.
"Kile unachosema ndicho kitakachotengeneza maisha yako, ukisema huwezi hutafanikiwa katika maisha, lazima tuseme tunaweza," aliwaasa.
Dk. Mengi alisema matumaini yake ni kwamba siku moja benki ya CBA iwe namba moja Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla.
Alisema uaminifu kwa wateja ndiyo huifanya benki ikue zaidi na kupiga hatua.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki ya CBA, Martin Mugambi, alisema
CBA ni ya kwanza iliyoanzisha huduma ya kadi maalum ya 'USD Credit Card' na inatoa dhamana ya mikopo mikubwa kwa wateja.
Kadhalika Mugambi alisema kwa kushirikiana na kampuni ya simu ya Vodacom kupitia M-pawa, mteja anaweza kuweka fedha kwenye akaunti ya simu kwa muda mrefu.
Katika maadhimisho hayo Taasisi ya Doris Mollel inayosaidia watoto njiti kupitia Mkurugenzi wake, Doris Mollel iliendesha harambee kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto hao na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. milioni 17.6.
Pia katika maadhimisho hayo kulitolewa zawadi mbalimbali kwa washindi wa shindano la mchezo wa gofu lililodhaminiwa na benki hiyo.
