Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini B jambo linaloathiri ukusanyaji wa damu katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Alisema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Kituo cha Damu Salama, Kanda ya Kaskazini kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Dk Ndugulile amesema, takwimu za ukusanyaji wa damu katika kanda hiyo zinaonesha kiwango kikubwa cha damu iliyokusanywa mwaka juzi na mwaka jana kimemwagwa baada ya kupimwa na kubainika kina maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini.
Amesema maambukizi ya ugonjwa wa ini yanaongezeka kwa kasi kubwa kuliko ya virusi vya Ukimwi (VVU) na kuwataka watanzania kujenga utaratibu wa kupima afya zao ili watakaokuwa hawajapata maambukizi wapewe chanjo.
Dk Ndugulile amesema kwa utaratibu wa kawaida, Serikali inatoa chanjo tano kwa watoto wadogo na moja ya chanjo hizo ni ya ugonjwa wa homa ya ini lakini watu wazima wanatakiwa kulipa gharama ili kupata huduma hiyo.
Amesema, maambukizi ya ugonjwa huo yanalingana na ya VVU na makundi ambayo yapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo ni watumiaji wa dawa za kulevya na wanaofanyakazi kwenye hospitali hasa maabara.
Dk Ndugulile alisema katika kuboresha upatikanaji wa damu, Serikali inatarajia kufunga mashine za kisasa na kujenga vituo 10 nchini kwa ajili ya kuhifadhi damu, lakini upimaji utaendelea kufanyika katika vituo vya kanda.
Kaimu Meneja wa Damu Salama kanda ya Kaskazini, Richard Komanga amesema, kumekuwa na ongezeko kubwa la wachagiaji damu wa hiyari kutoka asilimia 82 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 94 kwa mwaka huu.
Hata hivyo asilimia 3.5 ya damu iliyokusanywa mwaka juzi ilibainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini B, asilimia 1.3 homa ya ini C, VVU 1.8, kaswende 1.5, mwaka jana homa ya ini B 2.9, homa ya ini C 0.2, Kaswende 0.7 na VVU 0.8.
Alisema damu zinazokusanywa katika halmashuari mwaka juzi, asilimia nne ilikuwa na maambuki ya ugonjwa homa ya ini B , C 1.1 , Kaswende 1.5 , VVU mbili, mwaka jana asilimia 4.6 homa ya ini B , C 0.3 , Kaswende 1.6 , VVU 0.8.