Waziri Hasunga:Tumekusudia kufanya mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Kilimo


Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo ambapo Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo (ASLMs) na wadau wa kilimo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme Phase Two-ASDPII).
Katika utekelezaji wa ASDP II serikali imelenga kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (mazao, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 26 Novemba 2018 wakati akifungua warsha ya Wadau wa Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania inayofanyika katika Hoteli ya New Afrika Jijini Dar es salaam.

Alisema Utekelezaji wa lengo hilo ni kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kujitosheleza kwa chakula; kuimarisha uchumi; kuwa kichocheo cha kukua kwa viwanda; na kuongeza ajira ambapo ili kufikia malengo hayo; Utekelezaji wa ASDP II utazingatia mnyororo wa thamani wa mazao ya kipaumbele ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mhe Hasunga alisema kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima na wafugaji na kwa bei nafuu.

“Tumeanza na mbolea ambapo kwa sasa inaagizwa kwa pamoja na tumeondoa kodi na tozo nyingi katika mbolea ili ipatikane kwa bei nafuu. Kwa sasa changamoto kubwa imebaki kuwa gharama kubwa ya usafirishaji hasa kwa maeneo ambayo hakuna usafiri wa reli ambapo Serikali bado inalifanyia kazi suala hili” Alikaririwa Hasunga na kuongeza kuwa “Changamoto nyingine kama nilivyozitaja hapo awali tutaendelea kuzifanyia kazi na tunaomba wadau kupitia vyama vyenu na taasisi kilele kama Baraza la Kilimo, muendelee kutupa maoni yetu ya namna bora ya utatuzi na sisi tunaahidi kufanyia kazi maoni yenu”.

Kuhusu Masoko ya mazao ya kilimo, Hasunga alisema kuwa serikali inatambua changamoto za masoko, usindikaji, miundombinu ya umwagiliaji na miundombinu mingine kwa ajili ya mifugo na uvuvi, upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakati na kwa bei nafuu, uhaba wa maafisa ugani, kero za kodi na tozo mbalimbali, wingi na mwingiliano wa taasisi za udhibiti huku akiahidi kuendelea kuzitafutia ufumbuzi.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia