Waziri awataka Wananchi kulinda na kutunza vyanzo vya Maji


Na.Thabit Madai,Zanzibar.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Rashid Ali Juma amewataka Wananchi wa Donge Mnyimbi kutunza vyanzo vya maji na miti ili kudumisha matunda ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

Alisema kukata miti ovyo kunaondoa haiba ya mji na kupungua kiwango cha maji ambayo yanapotea kutokana na ongezeko la watu na matumizi makubwa ya maji hayo.

Waziri Rashid aliyasema hayo huko Donge Mnyimbi Wilaya Kaskazini B wakati wa ufunguzi wa mradi wa maji safi na salama ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 55 ya Mapinduzi  ya  Zanzibar .

Alisema azma ya Serikali kupitia ilani ya Chama cha mapinduzi pamoja na mpango wa kupunguza umasikini nchini  (MKUZA ) ni kuhakikisha Wananchi wa mjini na Vijijini wanapata maji safi na salama.


Aliwataka Wananchi wa Donge kuwa walinzi wa miundombinu hiyo na kuzithamini juhudi zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wafadhili ambao ni Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

“Mamlaka ya Maji (ZAWA) inahakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji safi kwa masafa mafupi na wananchi wana wajibu wa kuutunza vizuri mradi ili lengo lililokusudiwa liweze kutimia” alisema Waziri Rashid.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara Ardhi Maji Nishati na Mazingira Ali Halil Mirza amesema mradi huo umegharimu zaidi ya Dola za Kimarekani Million tano  ambazo ni ufadhil iwa Jamhuri ya Watu wa China .

Aidha alisema jumla ya shillingi milioni tano za kitanzania zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya malipo ya fidia na uvutaji wa umeme.

Alieleza vijiji ambavyo vitanufaika na mradi huo ni Donge Mbiji, Donge Mnyimbi, Donge Kirange, Donge Mtambile,Donge Kipange, Donge Vijibweni, Donge Mchangani na Muwanda .

Mradi huu ni  miongoni  mwa  miradi mitano ambayo imefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambayo imetekelezwa katika maeneo ya chaani kisongoni, kiboje na miwani utekelezaji wa miradi hiyo ilianza mwezi wa Juni 2016 na kukamilika April 2018.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia