Rais Dk. Shein afungua Skuli iliyogharimu Tsh. Bilioni 2


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amefungua Skuli ya msingi ya Fuoni /Pangawe, iliyopo Wilaya ya Magharibi B Unguja.

Ujenzi wa skuli hiyo uliogharimu zaidi ya shilingi Bilioni tano ni wa tatu kufanyika, ikiwa ni muendelezo wa misaada ya Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa Zanzibar, ikitanguliwa na ujenzi wa skuli za Kijichi na Urafiki iliyoko Mwanakwerekwe.

Dk. Shein amesema elimu ni fani inayokuwa na kuendelea siku hadi siku, hivyo ni vyema kwa walimu kwenda sambamba na mabadiliko hayo ili kukidhi haja ya zama hizi, akibainisha umuhimu wa kuwa na mbinu mpya za ufundishaji.

Alizitaka mamlaka zinazosimamia uendeshaji wa skuli hiyo kushirikiana na kuweka walimu wenye uwezo wa kitaaluma, wanaopenda kujituma na wenye kuweka mbele uzalendo ili ufanisi unaotarajiwa uweze kupatikana.

“Ni busara tukaiwacha ile tabia ya kuwafundisha watoto wetu yale tuliosoma sisi miaka iliyopita, tuelewe kuwa elimu si sawa na maji ya vidimbwi yanayotuama, bali ni fani inayokuwa na kuendelea siku hadi siku”, alisema.

Alisema ufunguzi wa skuli hiyo ni uthibitisho wa dhamira njema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu inayochochea maendeleo, ikiwemo ya elimu.

Aidha alisema ujenzi huo umetokana na mipango ya serikali, iliozingatia ripoti ya sensa ya watu na mkaazi ya mwaka 2012 pamoja an ripoti ya Utafiti ya watoto walio nje ya skuli.
Dk. Shein alibainisha kuwa ripoti hizo zimeonyesha ongezeko kubwa la idadi ya watu, jambo lililopasa kwenda sambamba na mahitaji ya kijamii, zikiwemo skuli na kusema kuwa Wilaya hiyo ina jumla ya watoto 36,666 wenye umri wa kati ay miaka sita na 11, ambao ni wajibu kwao kupata elimu ya msingi.

“Ripoti hizo zimebainisha kuwepo msongamano mkubwa wa wanafunzi unaofikia wastani wa wanafunzi 90 kwa darasa moja katika skuli za Wilaya hiyo, ikibainishwa ndio zinazoongoza katika changamoto ya aina hiyo”, alisema.

Rais Dk. Shein alisema uwepo wa skuli hiyo utasaidia sana upatikanaji wa nafasi za masomo kwa watoto wa maeneo hayo na hivyo kupunguza msongamano katika skuli za Kinuni, kijitoupelea, Chunga na Fuoni ambazo hivi sasa zina wanafunzi 17,054 ikiwa wastani wa wanafunzi 131 kwa darasa moja.

Dk. Shein aliipongeza Serikali ya watu wa China pamoja na Kampuni ya China Qindao Construction (CNQC) kwa kusaidia ujen zi wa jingo hilo zuri la kisasa na lenye viwango vinavyokubalika.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia