Naibu Waziri wa Nishati aridhishwa na maandalizi ya uzinduzi wa mradi wa umeme


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amesema ameridhishwa na maandalizi ya uzinduzi wa mradi mkubwa wa umeme wa Makambako - Songea, unaotarajiwa kufanyika leo, Aprili 6, 2019; Mgeni Rasmi akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumza, mara baada ya kukagua miundombinu ya Mtambo wa kufua umeme wa Songea, ambapo uzinduzi unatarajiwa kufanyika, Naibu Waziri alimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hamisi Mwinyimvua pamoja na viongozi wa TANESCO kwa maandalizi mazuri.

Alisema, moja ya mambo muhimu yaliyofanyika na ambayo ni ya kutia moyo ni uunganishwaji umeme kwa wananchi wa maeneo jirani yanayozunguka Mtambo huo.

Aliwataka TANESCO na REA kuendeleza utaratibu huo wa kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na miradi mbalimbali ya umeme nchini kote wanaunganishiwa nishati hiyo kwani ndiyo walinzi wa kwanza wa miundombinu hiyo.

Naibu Waziri alifuatana na Katibu Mkuu Nishati, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Raphael Nombo pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara na TANESCO.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items