Mbunge ahoji TBC kutoonyesha habari za Upinzani


Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sophia Mwakagenda amelalamikia kile alichokiita ubaguzi unaofanywa na Televisheni ya Taifa (TBC) kwa kutorusha habari za upinzani.

Akizungumza bungeni leo Mwakagenda amesema TBC imekuwa na ubaguzi wa kutoa habari za wapinzani na kwamba kila wakati wamekuwa wakitoa habari zinazowahusu wabunge wa upande mmoja wakati ni chombo cha Serikali.

“Jana niliuliza swali kwa Waziri wa Mawasiliano lakini Waziri wa habari alijibu, hii TBC ni mali ya walipa kodi lakini imekuwa haitendi haki, kila wakati sisi wapinzani tunabaguliwa kwa habari zetu kutotumika tatizo ni nini,” amehoji Mwakagenda.

Akijibu mwongozo wa Mwakagenda, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameiomba Serikali kulitazama jambo hilo huku akibainisha kuwa hata taarifa za wabunge wa CCM wakati mwingine hazitoki na badala yake hutoka za upinzani pekee.

Mbunge huyo ametolea mfano hotuba za upinzani na michango yao kwamba kila wakati hakuna kinachotolewa kwenye televisheni hiyo akisema hakuna usawa.

Katika ufafanuzi wake Dk Tulia  amesema jambo hilo lilitokea jana hivyo liko kinyume na kanuni za Bunge ambazo hutaka jambo lililotokea mapema ndio kuulizwa bungeni.