Video inayodaiwa kuwa ya Gwajima, Jeshi la Polisi kuchunguza


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), limeanza uchunguzi wa video ya ngono inayosambaa mitandaoni inayodaiwa kuwa ni  ya Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Taarifa ya polisi imetolewa leo kufuatia kusambaa kwa video hiyo inayodaiwa kuwa ni yake, ikimuonyesha akiwa faragha na mwanamke.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumatano, Mei 8, 2019 na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, imeeleza kuwa Mei 7,2019 kuna video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na watu wasiojulikana ikionyesha mtu anayefanana na mchungaji huyo akiwa na mwanamke asiyefahamika.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalumu limeanza uchunguzi wa video hiyo mara moja na linapenda kuwapa taarifa wananchi (kuwa) Gwajima siyo mtuhumiwa, ni muathirika wa tukio hilo kwani tukio hilo linaweza kufanywa na mtu yeyote kwa nia ya kutaka kuharibu heshima yake kwa jamii na waumini," amesema Mambosasa.