https://monetag.com/?ref_id=TTIb Serikali yapokea mashine 62 za kusafishia damu, dhamani yake ni Tsh. Bilioni 1.55 | Muungwana BLOG

Serikali yapokea mashine 62 za kusafishia damu, dhamani yake ni Tsh. Bilioni 1.55


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yaendelea kusogeza huduma za matibabu ya figo kwa kupokea jumla ya mashine 62 za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo na kuzisambaza katika Hospitali za Rufaa za mikoa nchini.

Hayo yamejiri mapema jana katika tukio la kupokea mashine hizo kutoka kwa kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief wakiongozwa na ubalozi wa Saudia Arabia nchini zenye jumla ya Tsh.  Bilioni 1.55, lililoongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.

Dkt Ndugulile amesema kuwa Serikali inaendelea kusambaza na kuboresha huduma hizi na kwa sasa zinapatikana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando, Hospitali ya KCMC na baadhi ya Hospitali binafsi.

"Sisi kama Serikali tumeendelea kuboresha hizi huduma, kwa sasahivi zinapatikana Muhimbili, Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando, Hospitali ya KCMC na baadhi ya Hospitali binafsi" alisema Dkt. Ndugulile

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kuboresha huduma hizi licha ya kuwepo changamoto ya idadi kubwa ya wahitaji wa huduma hizi huku akidai kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuna mashine 42 huku zikifanyika sesheni tatu kwa siku, na zinafanyika kwa sikusita katika kila wiki.

Aidha, Dkt Ndugulile amesema kuwa, msaada huo wa vifaa vitavyosambazwa katika mikoa tisa nchini ikiweko mikoa ya Tanga, Mwanza, Kigoma, Kagera, Arusha, Iringa, Mtwara, Unguja na Zanzibar, hali itayosaidia kupunguza gharama kwa kuwasogezea wagonjwa huduma hizo.

Mbali na hayo, Dkt. Ndugulile amesema kuwa ndani ya miaka mitatu Serikali imefanikiwa kupunguza magonjwa yakuambukiza kwa asilimia 50%, huku akikiri kuwa bado kuna changamoto kubwa katika kukabiliana na magonjwa yasiyo yakuambukiza kama vile kisukari, presha na figo ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na mitindo ya maisha.