Mambo yaliyozungumzwa Ikulu leo


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 22 Julai, 2019 amemuapisha Mhe. George Boniface Simbachawene kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Mhe. Hussein Mohamed Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi hao kwa uteuzi walioupata na amewataka kwenda kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kurekebisha kasoro zilizopo katika wizara zao ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Amemtaka Mhe. Simbachawene kuhakikisha fedha nyingi zinazoelekezwa katika masuala ya mazingira zinaleta matokeo ya kuboresha mazingira, vibali vya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) haviwi kikwazo cha uwekezaji na kutekeleza maagizo yanayotolewa na Serikali kwa wakati.

“Nakumbuka suala la mifuko ya plastiki limechukua muda mrefu, karibu miaka minne, nimetia saini halikutekelezwa, Makamu wa Rais akazungumza weee halikutekelezwa, Waziri Mkuu akazungumza Bungeni halikutekelezwa, mpaka mwishoni mwishoni hapa nilipotoa amri ya lazima ndipo likaanza kutekelezwa, sasa usiende kufanya hivyo wewe (Mhe. Simbachawene)” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mhe. Bashe kutekeleza kwa vitendo mawazo yake mazuri ambayo amekuwa akiyatoa Bungeni kuhusu sekta ya kilimo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali, kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kutumia kilimo cha kisasa na kupata masoko ya uhakika ya mazao ya kahawa na pamba ambayo hivi sasa yapo katika msimu wa mauzo.

Mhe. Simbachawene amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na ameahidi kushughulikia masuala ya fedha nyingi zinazoelekezwa katika mazingira kutoleta matokeo katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, kuwezesha wizara nyingine kimazingira na kuimarisha Muungano.

Pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli, Mhe. Bashe ameahidi kutekeleza ipasavyo majukumu yake kwa kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kilimo inatekelezwa huku akitambua kuwa kati ya asilimia 60 na 70 ya Watanzania wanategemea kilimo na kwamba uwepo wake Bungeni umemsaidia kujua changamoto nyingi zinazowakabili wakulima.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kukutana na wafugaji wa Tanzania ili kuzungumza nao juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa lengo la kuhakikisha mifugo mingi iliyopo hapa nchini inaleta manufaa yanayostahili.