Anayedaiwa kumuua mkewe kisha kumchoma moto awatishia waandishi wa habari Mahakamani


Mshtakiwa wa mauaji ya mke wake,Hamis Said Luongo(38) ambaye anadaiwa kumuua mke wae kisha kumchoma moto Naomi Marijani eneo  la Gezaulole Kigamboni ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa atafanya kitu kibaya kwa waandishi wa habari ambacho mahakama hiyo haitakitarajia.

Awali, Wakili wa  Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amedai mbele ya Mahakama hiyo kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Baada ya maelezo hayo, mshtakiwa Luongo alinyoosha kidole na kuiomba Mahakama hiyo kuwa kichwa chake kimechanganyikiwa hivyo atafanya kitu kibaya kwa waandishi wa habari ambapo Mahakama hiyo haitatarajia.

"Mheshimiwa nina kitu ambacho nataka nikueleze kuhusu waandishi wa habari ambao wamekuwa wakinipiga picha kuanzia chini hadi ndani ya mahakama, sasa nakueleza hivi nitakuja kuishangaza mahakama hii nitafanya kitu kibaya ambacho hamtakitegemea.”

"Kuna kesi ambayo inanikabili na sielewi hatima ya kesi yangu, hapa nilipo kichwa changu kimevurugika nina mawazo ya mtoto wangu na ninapofika hapa ndani nataka akili yangu itulie lakini hawa wapiga picha wananipiga picha sasa nawaeleza kuwa nitawafanya kitu kibaya ambacho Mahakama haitatarajia," amedai

Baada ya kauli hiyo, Wakili Wankyo alimueleza mshtakiwa huyo kuwa kupigwa picha ni hali ya kawaida na washitakiwa wote wanaofikishwa mahakamani wanapigwa picha na yeye siyo mtu wa kwanza hivyo awape uhuru waandishi wa habari wafanye kazi yao kuwa huru.