Makonda ajipanga kuwakomesha wanaume wanaowatelekeza wanawake


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amepanga kuzisajiri ndoa zote za mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na wanaume wanaowalaghai wanawake kimapenzi.

Bwana Makonda amesema kuna mpango wa kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo kwenye mkoa wake ili kupunguza utapeli wanaofanyiwa wanawake kwa kudanganywa kuolewa.

Kanzidata hiyo itahusisha usajili wa ndoa zote ili wanaume waliooa waweze kubainika na kuwanusuru wanawake wasitapeliwe na kuumizwa mioyo kwa kutegemea ndoa.

Makonda amesema pamoja na kanzidata hiyo atatumia mkutano wa SADC kupata uzoefu kutoka kwa nchi nyingine kufahamu namna gani wanakabiliana na utapeli wa aina hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kumekuwepo na malalamiko mengi ya wanawake kuumizwa hivyo wakati umefika wa kuanza kushughulikia."Tutaanza kuangalia na kupata uzoefu kwa wenzetu wa SADC ambao kama haya wanashughulikiaje na mkutano ukiisha tutajadiliana kama mkoa tunawezeshaje usajili huo," amesema.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amedai kwamba amekuwa akikutana na malalamiko mengi sana kutoka kwa wadada wa mkoa huo kwamba wamechoka kutapeliwa.

''Tunaompango mzuri tu wa kukutana na wadada walioumizwa, huwezi kuwa kiongozi afu unaongoza watu walioumizwa na kutapeliwa na vijana ambao wanaona raha tu, tunataka tufikie hatua mtu akioa anaandika kwenye database ya mkoa, ili mwanamke akitaka kuolewa anaangalia huyu jamaa kaoa au hajaoa'' amesema Makonda.

Makonda ameongeza kuwa, wanaoumizwa wengi ni kina dada kwa sababu wanawake wakipenda huwa wanapenda kweli na wao kuwa wahanga wakubwa wa matapeli.

Amesema atatumia mkutano wa SADC unaowajumuisha wakuu 16 wa nchi wanachama kujifunza mambo mbalimbali, ikiwemo suala la wadada kutapeliwa juu ya masuala ya ndoa, kwa kuangalia nchi zingine zinashughulika vipi na masuala hayo.

Hii si mara ya kwaza kwa mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salam, kujaribu kusaidia kutatua matatizo yanayowakumba wanawake jijini Dar es Salaam.