Na Thabit Hamidu,Zanzibar.
Mkuu wa mkoa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amemuagiza Mratibu wa mradi wa huduma za jamii Mijini(ZUSP) Makame Ali Makame kuongeza muda wa ufanyaji kazi katika ujenzi wa mradi wa miundombinu wa mtaro ya kupitishia maji ya mvua eneo la Mikunguni.
Akitoa agizo hilo wakati alipotembelea eneo hilo la ujenzi huo Mkuu huyo wa Mkoa alisema ujenzi wa miundombinu hiyo katika eneo hilo limesababisha kujitokeza kwa usumbufu mkubwa kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo na wafanyabiashara wa eneo hilo.
Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa ujenzi huo umepelekea barabara ya Mkunguni kufungwa kwa muda wa miezi miwili mpaka sasa na kwamba hali hiyo imesababishia usumbufu wa hali ya juu kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo.
"Kutokana na hali hiyo nina mwagiza Mratibu wa mradi wa huduma za jamii Mijini(ZUSP) Makame Ali kuweza kuongeza muda wa ufanyaji kazi ilikufikia masaa 24 ili kuweza kumaliza hatua ya utoaji wa vyuma katika mradi huu,"alisema Mkuu huyo wa Mkoa
Katika maelezo yake uongozi wa mkoa wake umekubaliana na wakandarasi wa mradi huo kuifungua barabara hiyo wakati wa sikukuu ya Idd Al Haj ili kuwapatia nafasi wananchi kuitumia katika siku za sikukuu hiyo.
"Tumeelezwa kuwa usumbufu wa kufunga kwa barabara hii inatokana na kuharibika kwa mitambo ya utoaji wa vyuma katika ujenzi huu ambapo iliwabidi wakakodishe Dar es Saalam hivyo tumeshuhudia mtambo huu umeweza kufanikiwa kuvingoa vyuma hivi kwa hiyo ni imani yangu kuwa barabara hii itafunguliwa hivi karibuni,"alisema
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo wa huduma za jamii Mijini(ZUSP) Makame Ali Makame alitaja sababu ambayo imesababisha kufungwa kwa barabara hiyo kwa kipindi cha muda mrefu ambapo alisema inatokana na hali ya mvua na mitambo ambayo ilishindwa kufanya kazi.
Alisema mpaka sasa mitambo minne ililetwa katika ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya kuchomoa vyuma ambavyo viliwekwa katika mtaro huo na hatimaye ikashindwa kufanya kazi.
"Baada ya kuona mitambo hiyo minne yote imeshindwa kufanya kazi ndipo tukaona sasa tusitishe ufanyakazi na tukaagiza mtambo mwingine wa tano Dar es Saalam na kama mnavyoona leo tumejaribu kungoa vyuma hivyo na vimewezekana hivyo leo tutaanza kazi hii,"alisema Mratibu wa mradi huo.
Alisema mkandarasi wa mradi huo ameomba kufungua barabara hiyo na kwamba kama itawezekana itumike barabara moja ili ujenzi huo uweze kufanyika kwa ufanisi.
