Simwangushi Rais, Bajeti ya nchi zaidi ya asilimia 20 inatoka kwangu - Waziri Jafo


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo amewataka vijana  kutochezea amani ya Nchi na Badala yake wawe Mabalozi Wazuri wa kutunza na kuenzi amani hiyo kwani ni Tunu kwa Taifa la Tanzania.

Waziri Jafo amesema hayo leo  jijini Dodoma katika maadhimisho ya siku ya vijana duniani ambapo amesema amani iliyoasisiwa na Marais wa Tanganyika na Zanzibar ni vigumu kuirejesha ikipotea hivyo vijana  ni nguzo Muhimu wa Kuitunza amani hiyo.

“Waasisi wa Taifa letu, Julius Kambarage Nyerere na Aman Karume walipambana sana na walitumia gharama kubwa kuhakikisha amani ya nchi yetu inapatikana na tukajipatia Uhuru, kilichobaki ni kirahisi sana ni kuiendeleza ,kuienzi na kuitunza amani ya Nchi Yetu  kwani ikipotea kuirudisha ni vigumu sana ,na wenye wajibu na nguvu kubwa wa kuinza ni ninyi vijana “amesema Jafo.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewataka vijana waliopewa nafasi  za Madaraka kufanya kazi na kuacha maigizo ili waache historia ya Taifa la Tanzania.

Waziri Jafo amesema ni vyema kwa vijana waliopewa dhamana ya kuliongoza taifa  kuwajibika vyema kuwahudumia Wananchi.

Pia amewataka  kuchangamkia fursa ya mikopo ambayo imekuwa ikitolewa na Halmashauri ambapo amedai kwa sasa kina mama ndio wamekuwa wakichangamkia fursa hiyo.

 “Igeni mfano wangu mimi simwangushi Rais, bajeti ya nchi zaidi ya asilimia 20 inatoka kwangu, vijana mkipewa nafasi fanyeni kazi.Usikubali ukiwa kama kijana lazima uache alama ili wakukumbuke,kijana sio sifa kukaa kiti kirefu halafu unasema kunyweni mpaka mikono idondoke, acha alama wekeni mifano kwa watu wengine,”amesema .

Aliendelea kwa kusema, "Vijana acheni maigizo  fanyeni kazi ya kuwasaidia Watanzania fanya kazi kwa ajili ya kuwahudumia watu,fanya kazi yako itangazike,tukifanya maigizo hatuwezi kulisaidia Taifa letu.Niwaombe vijana wenzangu tupambane,”.