https://monetag.com/?ref_id=TTIb Waziri Biteko apiga marufuku shughuli za uchimbaji Madini ya Bauxite | Muungwana BLOG

Waziri Biteko apiga marufuku shughuli za uchimbaji Madini ya Bauxite


Waziri wa Madini, Doto Biteko kulia akimsikiliza kwa umakini Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mazinde Juu wakati wa mkutano huo.


Waziri wa Madini Doto Biteko amepiga marufuku kuendelea kwa shughuli za uchimbaji wa madini ya Bauxite katika milima ya Bughai mpaka hapo utafiti wa athari za mazingira utakapofanyika.

Marufuku hiyo ameitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Magamba wilayani Lushoto wakati wa ziara ya kutembelea eneo hilo na baadae kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.

Amesema kuwa hakuna shughuli za uchimbaji zitakazofanyika mpaka hapo watakapoweza kupata majibu sahihi ya athari za kimazingira katika eneo hilo.
“Nimepiga mafuruku shughuli zote za uchimbaji kuendelea kwani nimeona kuna mashine kule za uchimbaji hivyo ziondoeni “amesema Waziri huyo.

“Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa wilaya naomba mlisimamie hili Lakini wakati tunaendelea kufanya hilo zoezi wale walikuwa na mashine pale lazima tujue ni wakina nani na wanapeleka wapi hiyo Bauxite “Alisema

Waziri huyo pia amemtaka Afisa Madini mkoa wa Tanga kufanya uchunguzi wa kiasi cha Madini kilichochimbwa ili kuweza kuwachukulia hatua wahusika wote waliochimba bila ya kufuata utaratibu kwa sababu hawajaruhusu uchimbaji kutoka wakati huo.

Awali akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella aliwataka wananchi kuwa wasikivu na kama kuna mahala wanahitaji ufafanuzi watapatiwa ili kuondoa sintofahamu kuhusiana uwepo wa madini hayo.

Alisema kwamba kumekuwa na haya madini watu wa madini watakuja kutoa elimu hapa na waziri amekuja kuja kuona haya madini na kuona namna ya kuyaendeleza.
Mkuu huyu wa mkoa alisema kama ipo sheria inasema nini na kama kuna suala la kisheria kwenye suala la uchimbaji lazima kuzingatiwe sheria na taratibu zilizopo kwa maslahi ya Taifa.

Awali akizungumza wakati wa ziara ya Waziri huyo Afisa madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga Zabibu Napacho alimueleza Waziri huyo kwamba kwenye maeneo waliopewa ruhusu ya uchimbaji kuna mgogoro ulioanza muda mrefu tokea mwaka 2001 mpaka sasa.

Alisema kwamba hilo linatokana na wananchi kuwa na uelewa tofauti kuhusiana na uchimbaji wa Bauxite kwa ujumla kutokana na kuona kama utaondoa uoto wa asili na kuchafua mazingira kwa hiyo wananchi hawajaukubali mradi huo

Afisa Madini huyo Mkazi alisema pamoja na kwamba wadau wenye leseni za uchumbaji walichukua juhudi za kufanya utafiti za kuangalia athari za mazingira lakini lengo lao halikutimia kwa sababu wakati wakiendelea na mchakato huo ukaingiliwa.
Hata hivyo alisema inaonekana halmashauri na serikali wanaukubali huo mradi lakini wachache hawana uelewa kuhusu mradi huo kikubwa wananchi wanapaswa kupewa elimu kuhusiana na uchimbaji huo.