Waziri Lugola awataka Maafisa Uhamiaji kuepuka rushwa


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka Maafisa Uhamiaji nchini, kuepuka rushwa na kutokuwanyanyasa wageni na hasa wawekezaji nchini.


Akizungumza katika kikao cha Maafisa Uhamiaji Waandamizi kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Uhamiaji (Trita), Mjini Moshi, leo, Lugola alisema wawekezaji ni watu muhimu katika maendeleo ya nchi, hivyo wanaposumbuliwa kwa kunyanyaswa bila sababu za msingi ni kuvunja misingi ya uadalifu.


Pia Waziri Lugola aliwataka maafisa hao waache kutoa PI (tangazo la kuondolewa mtu asiye raia nchini) zenye utata kwa maslahi binafsi bila kuzingatia athari ambazo nchi inazipata.

“Yapo malalamiko kwamba kuna wageni wanaingia nchini na kuwekeza kwa ubia na Watanzania, biashara inapokuwa inaendelea Watanzania huwazunguka wageni na kuwatengeneza mazingira ya kuwafukuza ili wapate fursa ya kumiliki hizo biashara na hapo ndipo Idara ya Uhamiaji hutumika, acheni hayo mambo kwa kuwa yanatuchafua kama taifa letu,” alisema Lugola.

Aliongeza kuwa, Rais John Magufuli anatafuta wawekezaji kwa nguvu na kuwahakikishia usalama wao na biashara zao lakini baadhi ya watumishi wa umma badala ya kusaidia jitihada hizi wao wanatumika kuwafukuza kwa dhuluma.

Alisema wageni hao wakishafukuzwa na wanaacha uwekezaji wao nchini ambao wanadhulumiwa huko waliko wanaisema nchi vibaya na kwa uzoefu huo wageni wengine hawawezi kuja nchini.

“Tujitathimini, tuzingatie sheria, kanuni, taratibu na miongozo yetu kwa kuzingatia maslahi ya taifa, pia nawasihi sana mumsaidie mheshimiwa Rais kutimiza ahadi zake kwa Watanzania ambazo amezitoa kupitia Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ahadi zake nyingine mbalimbali ambazo amekuwa akiahidi na kuzitekeleza,” alisema Lugola.

Aidha, Waziri Lugola kabla ya kukifungua kikao hicho kilichojumuisha Maafisa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, alisema kikao hicho kitakuwa chachu ya kudumisha maadili ya kazi, nidhamu, utii, na ushirikiano katika maeneo yao ya kazi ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya Idara hiyo ya Upendo, Mshikamano, Uwajibikaji na Kukataa Rushwa.

“Ni imani yangu kuwa, mtaendelea kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia Sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma katika utoaji wa huduma bora kwa Wananchi,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, alisema kikao hicho zitatolewa mada mbalimbali zitakazowasilishwa kuhusu rushwa na Kanuni za Uendeshaji za Uhamiaji za Mwaka 2018 ambazo ndio mwongozo wa utendaji kazi wa  Idara ya Uhamiaji.

“Kwa kuwa Idara yetu ya Uhamiaji inatoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo pasipoti, vibali vya ukaazi, pasi pamoja na viza, hivyo kupitia kikao hiki tutazingatia kikamilifu mada hizo kwa kuwa zitatusaidia katika kutoa huduma bora kwa maslahi ya Idara yetu, Wizara na taifa kwa ujumla,” alisema Dkt. Makakala.