Na Clavery Christian, Kagera
Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jeneral, Marco Elisha Gaguti amesema kuwa fursa za uwekezaji mkoani Kagera zipo tena fursa za kilimo chenye tija ambapo amesema kuwa hata watu wa kutoa mfano wapo na kuwataka viijana kuacha tabia ya kukaa vijiweni wakilalamika kuwa hamna ajira.
Brig, jenerali Gaguti amesema hayo baada ya kutembelea shamba la muwekezaji mzawa ambaye amewekeza katika kilimo cha kisasa kilimo ambacho kina tija na kinachotumia mitambo na vifaa ya kisasa katika kulima.
"Mradi huu kwangu ni mradi muhimu kwasababu umejumuisha mwekezaji mzawa aliyepewa uwezo na bank ya kilimo Tanzania TADB lakini kubwa zaidi ni mipango iliyopo, kwanza ya kupata uzalishaji mkubwa wenye tija na kuongeza thamani ya mazao ambayo yatapatikana katikana mashamba haya ambayo tumeyaona" alisema Rc Gaguti.
Rc Gaguti amesema kuwa amefuraishwa na ushirikiano uliopo kati ya mwekezaji huyo na wanakijiji wanaomzunguka ambapo amesema kuwa maandalizi yake ni mazuri ya vifaa kwa ajiri ya kuwashirikisha wananchi wa kawaida kufanya kilimo chenye tija na kuwa na uhakika wa masoko ya nje nchi na ndani ya nchi. Aidha Rc Gaguti amesema kuwa taifa pia litapata tija kwasababu faida yote itakayopatikana itabaki Tanzania na kulinufaisha taifa tofauti na mwekezaji wa kigeni.
Kwa upande wake mkurugenzi wa mradi wa global agency amesema kuwa amefurahishwa na ujio wa mkuu wa mkoa kwasababu umekuwa na neema kwake ambapo amemuhakikishia ushirikiano wa kutosha kutoka kwake ambapo amemuondolea hofu katika swala la kupata umeme swala alilokuwaanaisi atasumbuka sana kuletewa umeme.
Bw. Fidelis Christian Bashasha amesema kuwa alianza uwekezaji katika kilimo cha kisasa miaka sita iliyopita na amekuwa akipata ushirikiano wa kutosha katika uongozi wa Serikali ya Mkoa na Wilaya na hajawahi kupata changamoto yoyote wakati akiandaa mashamba yake na sehemu ya kujenga kiwanda Omukajunguti.
“Tayari tumefanya majaribio ya mazao matatu ambayo ni mpunga mweupe, alizeti na mahindi, mazao hayo yanakubali kwa eneo la shamba letu na kazi ya kuondoa maji na kufanya ulinganisho wa shamba umekalilika mwaka huu tumelima ekari 3000 kwa msimu huu wa vuli na tunatarajia kuvuna zaidi ya tani 120 na tumepata soko nchini Rwanda wanahitaji tani 30,000.” Alieleza Bw. Bashasha
Bw. Bashasha anajenga kituo cha kukusanya mazao yakiwemo ya wananchi na kituo hicho kitakuwa na kiwanda cha kukausha na kusindika mazao hayo kabla ya kusafirishwa na kupelekwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

