Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wote nchini, aliowateua kuhakikisha wanajifunza namna ya kutatua kero na migogoro ya wananchi, badala ya kumuachia yeye na Waziri Mkuu, kwa sababu wao si malaika.
Aidha, ameagiza kuanzia sasa watumishi wote watakaoharibu katika kazi zao, wakiwemo maofisa wa polisi, wasihamishwe, bali wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Sambamba na hayo, amemtaka Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuwasambaza watalaamu wa maji mikoani, badala ya kuwaacha mijini.
Ameendelea kuonesha kukasirishwa na kitendo cha Mkoa wa Rukwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliopatiwa mimba, na kuwataka wanafunzi kuacha tama, huku akiagiza viongozi wa mkoa huo ikiwemo jeshi la polisi kujipanga upya.
Ameyasema hayo Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua miradi mbalimbali ikiwemo ya maji, barabara, hospitali ya wilaya na kituo cha afya.
Alisema anasikitishwa na kitendo cha kuona wananchi katika kila ziara zake, wanakuwa na mabango mengi yenye matatizo, ambayo yanaweza kutatuliwa na viongozi wengine wa chini yake.
"Hebu jifunzeni namna ya kusikiliza migogoro ya wananchi, hii leo hapa kusingekuwa na mabango mengi kama haya. Wasikilizeni wananchi. Haiwezekani kero zote zimalizwe na Waziri Mkuu au Rais,"alieleza.
Alisema kuna migogoro inaweza kutatuliwa na mwenyekiti wa kijiji, katibu tawala wa wilaya (DAS), mwenyekiti wa wilaya, mkuu wa wilaya, mkuu wa kituo cha polisi, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), mkuu wa mkoa, viongozi wa dini n ahata viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
"Nawaomba viongozi wote na wa chama changu (CCM) shirikini katika kutatua migogoro ya wananchi, hata ningekuwa malaika siwezi kutatua migogoro yote," alisisitiza.
